Ukweli kuhusu ‘THE DA VINCI CODE’ Riwaya ya Kashfa dhidi ya imani ya Kikristo (4)
Siri ya Kashfa dhidi ya Yesu ni kupinga Uungu wake

Leo tunahitimisha Hoja yetu, Ukweli kuhusu ‘THE DA VINCI CODE,’ Riwaya ya Kashfa dhidi ya imani ya
Kikristo, kwa kuangalia jinsi Mwandishi alivyopindisha ukweli kwa nia ya kupinga uungu wake. Hata hivyo,
Maandiko Matakatifu yako wazi kuwa Bwana Yesu hakuoa kwa sababu alikuwa Mungu asilimia mia moja,
kulingana na ushahidi wa Biblia takatifu tunayoiamini. Mpenzi msomaji wangu, mwisho wa makala haya ya
‘THE DA VINCI CODE’ ndiyo mwanzo wa maandalizi ya makala nyingine, kwa lengo la kuelimishana katika
mambo ya kiroho na kimwili pia. Sasa endelea...

Tangu mwanzo wa huduma ya Yesu Kristo mpaka alipokufa na kufufuka katika wafu kisha akapaa mbinguni, wanafunzi
wake walikuwa wakimpa heshima ya uungu, sawa na Mungu kama alivyojitambulisha kwao yeye mwenyewe. Kwa hiyo,
kabla ya hata ya mfalme Constantine kuitisha mkutano wa Nikea, wakristo walikuwa wakimwabudu Yesu kuwa ni Mwokozi
na Mungu.

Hata hivyo, mnamo karne ya nne, aliibuka mzushi mmoja jina lake Arius aliyeanzisha kampeni ya kile alichokiita kutetea  
umoja wa kuwa ni nafsi moja na akaanza kufundisha kwamba Yesu hakuwa Mungu, bali naye ni kiumbe, japokuwa ana
hadhi zaidi ya malaika, lakini si Mungu. Lakini Athanasius na viongozi wengi wa Kanisa walisimamia vikali kuwa Yesu
alikuwa ni Mungu katika mwili.

Mfalme Constantine akitaka kusuluhisha mgongano huu ili kuleta amani katika himaya yake na kuondoa mgawanyiko
kati ya Mashariki na Magharibi, mnamo  mwaka 325 B.K. aliitisha mkutano wa Maaskofu 300 huko Nikea waliokusanyika
kutoka kila mahali duniani.

Kwa hiyo, kama nilivyokwisha kudokeza huko nyuma kwamba wanafunzi wa Yesu waliamini kwamba Yesu ni Mungu
badala ya kuwa kiumbe. Hii ilitokana na mtume wake wa kwanza kuandika vitabu na nyaraka za kwanza kuhusu maisha
ya Yesu zikimtaja Yesu ni Mungu.

Tunaporejea madai ya kitabu cha ‘The Da Vinci Code’ kinachodai kwamba madai ya uungu wa Yesu yalitengenezwa na
kuingizwa katika maandiko mnamo karne ya nne, ndipo tunapogundua kwamba siri ya kashfa dhidi ya imani ya Kikristo
imelenga kupinga moja kwa moja uungu wa Yesu.

Mwandishi wa kitabu hicho, Bw. Brown anatetea uzushi wa Arius. Aidha, Bw. Brown hakutaka kusema ukweli kwamba
katika mkutano wa Nikea,  tamko la kuendelea kukiri uungu wa Yesu liliungwa mkono na Maaskofu 318 na kwamba ni
wawili tu ndio waliokataa kukubaliana na maamuzi ya kikao hicho. Wakati Arius aliendelea kuamini kwamba Nafsi ya
Baba ndiyo ilikuwa ni Mungu peke yake na kwamba Yesu alikuwa kiumbe wake mkuu, Baraza la Maaskofu wengine
walishikilia msimamo wa Nafsi tatu za Mungu ambazo ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Hii inadhihirika katika tamko la
imani ya Nikea linapotetea uungu wa Yesu pamoja na Roho Mtakatifu.

Kuzaliwa kwa Yesu na Mariamu si mwanzo wa kuwepo kwake

Habari za Yesu kujulikana kuwa ni Mungu zililetwa na Malaika Gabriel kwa Mariamu. Katika ufafanuzi  malaika Gabrieli
aliweka bayana kwamba huyo ambaye angezaliwa duniani ni Mwana wa Mungu aliye juu: “Tazama utachukua mimba na
kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana
Mungu atampa kiti cha Enzi cha Daudi, Baba yake.” (Luka 1:32).

Mtu wa pili kutaja habari za uungu wa Yesu ni Yohana Mbatizaji aliyetangulia kutabiri habari za kuja kwake. Hii
inadhihirishwa na pale ambapo Yesu alipotaka kubatizwa na Yohana alitaka kukataa akisema hastahili kumbatiza:
“Lakini Yohana alitaka kumzuia, mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? (Mat.3:14).
Wapinzani wa uungu wa Yesu hujikwaa katika historia ya kuzaliwa kwa Yesu katika mwili, wakidhani huko ndiko mwanzo
wa kuwepo kwake. Lakini maandiko yanadhihirisha kwamba kabla ya Kristo kuja duniani, alikuwepo kabla! Ndiyo maana
wakati Yesu anajadiliana na Mafarisayo kuhusu habari za Ibrahimu ambaye walimwamini kuwa ndiye baba wa imani
kwao, yeye akasema alikuwepo kabla ya Ibrahimu hajakuwepo: “Yesu akawaambia, Amin amin nawaambia, yeye
Ibrahimu asijakuwapo, mimi niko.” (Yoh.8:58)

Ushahidi kamili ni jinsi Yohana alivyoanza kuandika habari za Yesu. Tofauti na Waandishi wa Injili za Mathayo, Marko na
Luka, Yohana alianza kwa kuandika kuwepo kwa Neno ambaye hatimaye anataja alikuwa ni Mungu: “Hapo mwanzo
kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.
Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. (Yoh.1:1-13)

Aidha, Yohana ndiye anayefunua kwamba huyu Neno ambaye alikuwa Mungu na alihusika katika uumbaji wa vitu vyote,
ndiye alikuja duniani na kufanyika mwili: “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu, nasi tukauona utukufu wake kama
wa Mwana pekee atokaye kwa Baba amejaa neema na kweli” (Yoh.1:14)

Mwisho kabisa, tunasoma habari za Yesu alipomtokea Yohana huyu huyu, alipokuwa ametupwa katika kisiwa cha Patmo
kama mfungwa wa dini. Hapo ndipo Yesu anajitambulisha kwake tena kwa sifa ya Mungu mwenyewe: “Mimi ni Alfa na
Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.” (Ufu.1:8)

Yesu hakuoa kwa sababu alikuwa Mungu

Katika kuhitimisha makala haya, naweza kusema kwa ujasiri kwamba Yesu hakuja duniani kuoa na kuzaa, kwa sababu
hakuwa binadamu kwa asili. Alivaa mwili wa binadamu kwa sababu ya ukombozi wa binadamu kutoka katika dhambi.

Na hii ndiyo inamtofautisha Yesu na manabii au mitume wa dini zote duniani. Yeye alikuwa Mungu kabla, ni Mungu hata
sasa na ataendelea kuwa Mungu milele. Wazushi wote waliotangulia na wanaoendelea mpaka sasa akiwemo Brown na
kitabu cha ‘The Da Vince Code,’ wametumiwa na Ibilisi kutaka kumfanya Yesu kuwa binadamu wa asili. Nia ni kuwafanya
binadamu waondoe imani yao kwake wasimwamini kuwa ni Mungu mwokozi wao. Hakuna uongo mpya kwa sababu Ibilisi
ambaye ni baba wa uongo hajabadilika.

Mwisho, ningependa kusema kwamba uungu wa Yesu si wa kupewa, bali ndiyo asili yake. Kila mwenye kutaka
kuthibitisha uungu wake anaweza kukutana naye binafsi akajitambulisha kwake kama alivyojitambulisha kwa wanafunzi
wa kwanza. Maana Yesu ni yeye yule jana, leo na hata milele.