Je, ni kweli Serikali ya awamu ya nne ina udini? (2)

Tusijenge hofu isiyo na ushahidi

Pamoja na kwamba kusema ni sehemu ya haki na uhuru wa kutoa maoni binafsi, lakini lazima
tupime mapema kwamba maoni yetu yatakuwa na athari gani kwa jamii. Kama
nilivyotahadharisha kwamba si sahihi kudai kwamba kwa kuwa kuna waislamu wengi ambao
wanateuliwa kushika madaraka ya juu ya uongozi, basi huo ndio udini.

Aidha, pia nilisema kwamba inawezekana hata sisi wenyewe kuonesha hisia za kutokutaka
waislamu wengi kushika madaraka ya uongozi wa juu kukatafsiriwa na waislamu kuwa ni udini!
Hata hivyo, hoja yangu ya msingi hapa ni kutahadharisha kwamba hisia hizi tukiziachia
zikaendelea kuzagaa katika jamii, tayari tunajenga hofu, tena hofu ya udini.

Watanzania katika enzi hizi za Karne ya 21 tukianza kuishi maisha ya hofu za kidini, tujue
tayari tunazidi kujikwamisha wenyewe kiuchumi na kimaendeleo. Isitoshe, hata utendaji wa ‘Ari
mpya, nguvu mpya na kasi mpya,’ nao pia utaathiriwa na hofu hizi na hivyo kushindwa kufikia
malengo yaliyokusudiwa kwa kila Mtanzania kuwa na maisha bora.

Kwa mujibu wa imani ya Kikristo, hususan kwa wakristo wenye kujua na kuheshimu Maandiko
Matakatifu ya Biblia, tumeambiwa kuwa  hatukupewa ‘roho ya woga’. “Maana Mungu hakutupa
roho ya woga, bali ya nguvu na upendo na moyo wa kiasi.” (2 Tim.1:7)  Kwa nini tuanze kuishi
maisha ya hofu kama watu wasioamini kabisa! Tunaagizwa kuishi kwa upendo na moyo wa
kiasi. Hapa moyo wa kiasi una maana ya kuwa na akili zilizotulia, zisizoyumbishwa yumbishwa.
Ni pamoja na kuwa na mawazo yasiyo kinyume bila sababu.

Tusijenge chuki za ubaguzi wa kidini

Ikiwa tutaendekeza hizi hofu za kidini sio kwamba zitatuathiri kiuchumi peke yake, lakini pia
zitachochea na kuhamasisha chuki na ubaguzi wa kidini katika jamii. Muda si mrefu sana
tayari Tutajenga chuki miongoni mwa waislamu na wakristo katika jamii, hali ambayo ni hatari
kwa amani na utulivu wa taifa letu.

Mimi naogopa kwamba tukiendekeza vichuki vidogo vidogo tunaweza kufikia kiwango
ambacho kila mkristo akimwona muislamu na kanzu na barakashia yake kichwani, tayari
anajisikia vibaya. Kusema kweli haya si maisha mazuri kwa mtu aitwaye mkristo hata kidogo.
Na wala tusijidanganye kwamba kutokufurahia kuona mtu wa dini nyingine anafanikiwa ndio
kuutetea ukristo kiimani. Si kweli hata kidogo.

Narejea kusema tena kwamba, chuki ya aina yoyote (ukiondoa hisia ya kuchukia maovu), ina
athari kubwa katika jamii. Chuki huondoa uhusiano mwema na ushirikiano katika jamii. Chuki
ni hisia kali ambayo kila mwenye kuwa nayo, kila mara huwaza kinyume cha mambo dhidi ya
yule anayemchukia. Hata kama likifanywa jambo jema kiasi halitapokewa kwa sababu tu
mtendaji hakubaliki.
Tusisahu kwamba idadi ya waislamu na wakristo hapa nchini inawiana kiasi kwamba,
tukiruhusu aina yoyote ya udini, madhara yake ni makubwa sana. Katika nchi ambazo watu
wanaobaguliwa ni wachache, athari hizo huishia kwa wenye kubaguliwa. Lakini katika nchi
ambazo wanaobaguliwa ni wengi, athari hizo huwapata hata wabaguzi wenyewe. Tanzania
haiwezi kupona hata kidogo kama chuki na ubaguzi wa kidini utashamiri. Yanayotokea Sudan
ni madogo sana.

Tusiwape wakati mgumu waislamu walioko madarakani

Haipendezi wala haifai pale ambapo tutaanza kuwapa wakati mgumu waislamu walioteuliwa
kushika madaraka ya uongozi kwa kuwajengea  hisia kwamba wamepewa nafasi hizo kwa
misingi ya udini. Nasema huku ni kuwapa wakati mgumu kwa sababu kwanza hawakujiteua
wenyewe na pili aliyewateua ana imani na utendaji kazi wao.

Pengine nitoe tahadhari yenye msisitizo mkali zaidi kwa kusema kwamba, tusiwajengee hisia
za kidini ambazo wakati walipoteuliwa hawakuwa nazo! Kimsingi, ‘ukimbagua’ mtu kwa sababu
yoyote, matokeo yake naye pia hupatwa na ile hisia ya ‘kubaguliwa’. Sasa ikiwa hisia hiyo ya
kubaguliwa itamzidi hata akashindwa kuitawala, si ajabu akaanza naye kujihami (kwa kesi hii
akaanza kuonesha udini), mbegu ambayo atakuwa ameingiziwa kutokana na kubaguliwa kwa
sababu ya dini yake.

Kama nilivyotangulia kushauri hapo awali, tuwaache huru waislamu walioteuliwa kushika
madaraka ya uongozi wa nchi. Aliyewateua tunamwamini. Tusubiri tuone utendaji wao. Ikiwa
kweli watathibitika kwamba hawatimizi wajibu wao kwa wananchi wote isipokuwa kwa waislamu
wenzao tu, hapo tutakuwa na mahali pa kuanzia kusema.

Ninafahamu kwamba si wakristo wote wenye hisia kinyume na uteuzi wa Waislamu kushika
madaraka ya uongozi. Hata hivyo, hata kama ni wachache wenye hisia hizi, bado hatuwezi
kuwapuuza kwa sababu ‘chachu kidogo huchachua donge zima’.
MAKALA ILIYOPITA YA 1
Jifunze na kusoma kwa makini maoni ya wengine