Je, ni kweli Serikali ya awamu ya nne ina udini? (3)
WIKI iliyopita nilizungumzia kuacha tabia ya kujenga hofu kuhusu tuhuma zisizo na ushahidi kamili,
nikatahadharisha kujiepusha kuendeleza chuki za ubaguzi wa kidini na kwamba tusiwape wakati mgumu
wale walio na watakao teuliwa na Rais kushika madaraka ya uongozi wa juu katika nchi. Leo napenda
kuelezea zaidi kuhusu nafasi ya Ukristo katika awamu ya nne ya utawala uliopo madarakani:
Hivi ‘udini’ tunautambua kwa majina ya kidini tu?
Tangu nimeanza kusikia kuhusu matumizi ya neno ‘udini,’ nimekuwa nashindwa kuelewa linapotajwa linamaanisha nini
hasa. Nimekuja kugundua kwamba huenda neno hili ‘udini’ lina tafsiri nyingi na kila mara litajwapo tusipotafuta tafsiri iliyo
rasmi, tunaweza kupotoshana na kutafunana wenyewe kwa wenyewe kwa ujinga wetu.
Haya niyasemayo hapa nachokoza katika kutafuta kujua tafsiri ya ‘udini’ unaodaiwa kuwepo katika Serikali ya awamu ya
nne, maana yake ni nini? Hivi tunautafsiri udini kwa kuangalia majina ya dini wanakotoka? Kwamba akiitwa Juma ni
Muislamu na akiitwa Mathayo ni Mkristo? Nasikitika kusema kwamba kama kweli kigezo chetu ndio hiki, basi uelewa wetu
kuhusu ‘udini’ utakuwa umeshuka viwango vinavyostahili!
Nasema hivi kwa sababu kuna watu wanatumia majina ya kiislamu, huku tayari ni wakristo kwa imani zao na hali
kadhalika kuna watu wanatambulikana kwa majina ya kikristo wakati ni waislamu kwa imani yao. Kuna waislamu
waliobatizwa kuwa Wakristo, lakini wakaendelea kuitwa majina ya Kiislamu na wako baadhi ya wakristo waliosilimu
wakaendelea kuitwa majina ya Kikristo!
Je, majina ya kidini ndio ushahidi kwamba wahusika ni waumini waaminifu katika dini zao? Nijuavyo dini zote mbili
zinakataza maovu katika jamii. Lakini hebu nenda magerezani uone wafungwa waliohukumiwa adhabu kwa sababu za
maovu waliyotenda, utawakuta wote wenye majina ya kidini wamo. Kuna akina Yohana na akina Zuberi.
Hivi tunaweza kwenda magerezani na kuanza kuhesabu wafungwa kwa majina yao, kisha tukikuta idadi kubwa ya
wafungwa wanatoka dini moja tutasema kuna ‘udini magerezani’? Tutaanza kuwalalamikia mahakimu na majaji kwamba
wanatoa adhabu kwa kupendelea watu wa dini moja, dhidi ya dini nyingine? Je! Tuanze kuwashauri mahakimu na majaji
kabla ya kutoa hukumu ya adhabu kwa wahalifu wazingatie uwiano wa kidini? Najua utaniona nafanya mzaha kwa
kusema haya. Lakini ukweli wa mambo hapa ndipo tulipofikia!
Sijasema kwamba jina la mtu halihusiki katika kumtambulisha dini yake. Lakini napinga kutumia kigezo dhaifu kumtafsiri
mtu kuwa ni ‘mdini’ kwa sababu tu ya jina lake. Maana hapa hofu yetu ni kuwa majina ya watu kutoka dini moja yakizidi
kwenye safu ya uongozi wa nchi, ati tayari huo ndio umegeuka kuwa ‘udini’! Kama hiki ndicho kigezo, basi tutakuwa
tunahalalisha pia madai ya baadhi ya vikundi vya kidini ambavyo huko nyuma vilisema sana kwamba nchi hii inatawaliwa
Kikristo, ati kwa sababu walioko madarakani wengi wana majina ya Kikristo!
Ombi langu kwa wakristo wenzangu ni hili, tusiingie katika mtego wa ubaguzi wa kidini. Hii si itikadi ya Ukristo kwa asili
yake. Yesu Kristo mwenyewe hakuwa na wala si mtu wa tabia hii. Kama unamwona mtu mwenye jina ambalo si la
Kikristo, kisha ukaanza kujisikia vibaya, basi huo ndio unaitwa ubaguzi wa kidini. Siku hizi kuna neno limeshika hatamu
kuhusu ‘ubaguzi’ ambalo ni ‘unyanyapaa’! Tusiwanyanyapae watu wa dini nyingine kwa visingizo visivyokuwa na
ushahidi.
Siri ikisha fichuka sio siri tena
Kwa kusema haya naomba kueleweka kwamba sikatai kabisa kuwepo kwa hisia za watu wa dini moja kutaka kuitawala
nchi kwa misingi ya udini. Hisia kwamba kuna njama za kutaka kuigeuza nchi hii kutawaliwa kwa misingi ya udini
hazikuanzia leo. Zimekuwepo tangu Serikali ya awamu ya kwanza mpaka leo hii. Hapa sipendi kuanza kutaja maeneo
ambayo watu wanayatafsiri kuwa ni njama za kuitawala nchi kidini. Nadhani haya yanahitaji makala yake tofauti na si
vizuri kuchanganya mada.
Lakini ninachotaka kusisitiza hapa ni kwamba, kanuni ya siri ni pale ambapo haijajulikana nje ya wanasiri wenyewe.
Lakini siri ikisha fichuka sio siri tena. Ikiwa kile ambacho kilikuwa ni siri kimejulikana hadharani, maana yake hata mbinu
za utekelezaji wake lazima zibadilike pia. Kwa mfano, watoto wana mchezo wa kitoto, mmoja wao kujificha mahali ili
kuwatishia wenzake.
Ili mchezo huu ufaulu, lazima mhusika ajifiche kweli kweli na asigundulike mahali alipo. Baada ya wenzake kukaribia
mahali alipo, ndipo hujitokeza ghafla kwa kishindo cha sauti na kushtua wenzake. Lakini iwapo yule aliyejificha
atagundulika mahali alipo mapema kabla hajatimiza azma yake, hata kama akijitokeza kwa kishindo, hatawashtua tena
wenzake! Amechelewa na mchezo umekufa.
Njama zote zilizobuniwa au zinazoweza kubuniwa na kutaka kutekelezwa kwa misingi ya kuitawala nchi kidini, ninazitafsiri
kama mchezo wa kujificha, kisha kugundulika kabla ya kutimiza azma yake. Hata kama njama hizo zimesukwa ili
wahusika wakiwa wengi wafanye maamuzi ya kisingizio cha ‘Demokrasia’, tayari mpaka sasa kila upande unajua na hisia
za watu katika suala hili ni kali.
Ndiyo maana nilisema huko nyuma kwamba, kutokana na mabadiliko makubwa ya kisiasa, kisayansi na kiteknolojia,
hakuna njama yoyote iliyo kinyume na maslahi ya Watanzania walio wengi inayoweza kutekelezwa pasipo kugundulika
mapema.
Ukweli kuhusu takwimu za uteuzi wa Rais Kikwete
Kumhusisha Rais Kikwete na upendeleo kwa Waislamu ni uzushi wa kihaini wenye lengo la kuiangamiza nchi yetu.
Rekodi ya uteuzi uliokwisha fanywa na Rais Kikwete inaonesha kinyume chake kabisa. Mawaziri wote ni 29. Kati yao
Wakristo ni 15 na Waislamu ni 13. Waziri mmoja yeye anasema hana dini. Naibu Mawaziri wote ni 33 na kati yao wakristo
ni 22, ukilinganisha na waislamu 11, idadi ambayo ni mara mbili. Makatibu Wakuu walio wakristo ni 20 na waislamu ni
wanane. Naibu Makatibu Wakuu wakristo ni 11 ukilinganisha na waislamu watatu tu. Rais ameteua Wakuu wa Mikoa
Waislamu nane na wakristo 13.
Ikumbukwe Makatibu Wakuu ndio watendaji wakuu wa Serikali na ndio walio na mamlaka ya kuajiri na kufukuza watendaji
wengine wote Serikalini na taasisi za umma. Katibu Kiongozi ambaye ndiye mkuu wa utumishi wa umma ni mkristo, hata
Katibu Mkuu (Ikulu) ni mkristo. Hivyo, haiingii akilini kudai kuwa Kikwete anapendelea waislamu.
Baada ya miaka zaidi ya 40 kupita bila Watanzania kuwa na dhana hiyo ya upendeleo kwa misingi ya dini, ni vigumu
leo hii ikatumiwa dini kuhoji uteuzi wa viongozi serikalini kwani haipo kabisa akilini mwa wanaofanya teuzi mbali mbali,
akiwemo Rais wa nchi. Rais Kikwete aliapa kuitekeleza na kuitetea Katiba ya nchi na kufuata sheria zake. Sheria ya
Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 inaeleza vizuri vigezo vinavyotumiwa kwa uteuzi na ajira.
IDADI WAISLAMU WAKRISTO HANA DINI
MAWAZIRI 29 13 15 1
NAIBU MAWAZIRI 33 11 22 -
MAKATIBU WAKUU 28 8 20 -
NAIBU
MAKATIBU 14 3 11 -
WAKUU
WAKUU
WA MIKOA 21 8 13 -
JUMLA 125 43 81 1
Tusiyumbishwe na wapenda fujo
Napenda kuwasihi sana wakristo na waislamu kwa ujumla kwamba tusikubali kuyumbishwa na watu wachache wapenda
fujo na vurugu. Watu hawa wachache wanaweza kujiita ‘manabii’ au ‘mitume’ waliotumwa na Mwenyezi Mungu kuanzisha
vurugu katika jamii. Lakini lazima tukubali kwamba katika kila jamii, hapawezi kukosekana watu ambao kwa hulka zao,
kazi yao kuu ni kuchochea hisia mbaya zenye kuleta mgawanyiko miongoni mwa watu.
Hata kama watu hawa ni wachache, lakini usumbufu wao huwafikia walio wengi. Mara nyingi watu wa jinsi hii huwa
wamejaribu kufanya mambo mengi ya maana na ya kimaendeleo, lakini kwa sababu mbali mbali, walishindwa au
hushindwa kufikia malengo yao. Cha kushangaza zaidi ni kwamba, badala ya wao kuzidi kutafuta njia mpya za
kujikwamua kimaisha ambazo hazitawahusisha wengine kwa ubaya; badala yake ‘kushindwa kwao’ huwasukuma kuanza
kutafuta jinsi ya kuharibu mafanikio ya wengine waliofaulu kufikia malengo yao, kijamii na kimaisha.
Watu wa jinsi hii, naweza kuwaita ‘wanaharakati walioshindwa’ kufanya mema ya kuwafaa wengine, na badala yake
huamua kujivika ‘ushujaa wa kuharibu’ mambo ya wengine, kwa kisingizio ama cha ‘kujitoa mhanga kutetea haki’ au
kuwa tayari ‘kufia dini’ na mambo mengi yanayofanana na haya.
Mara nyingi hawa ‘wanaharakati walioshindwa’ wanaweza kuamua kusema lolote dhidi ya yeyote, bila kuogopa
chochote, ili mradi tu wajulikane kuwa wao ni mashujaa! Usipowapima kwa makini unaweza kutekwa nao kwa sababu
baadhi ya hoja wanazosimamia zina ‘nusu ukweli’! Lakini ukweli wa mambo, nia zao za ndani za kuanzisha fujo na
uchochezi uwe wa kidini au kisiasa, ni kwa sababu wanajua kwamba mambo yakiharibika katika jamii kwa fujo zao; wao
hawana kitu chochote cha maana cha kupoteza kwa sababu hawakuwahi kuivisha chochote katika maisha!
Tusiyumbishwe na harakati zao za kueneza chuki za kidini au kisiasa.
Jifunze na kusoma kwa makini maoni ya wengine
|