Je, ni kweli Serikali ya awamu ya nne ina udini? (4)
Jumapili hii napenda kuhitimisha hoja hii. Hii haina maana kwamba nimemaliza yote niliyokuwa nayo kuhusu
suala la udini. Lakini nadhani kwamba yale niliyosema yanatosha kwa wale wenye busara watakuwa
wameelimika. Yaliyomo katika makala haya yanawalenga wale wote ambao wanapenda kutumia hekima na
busara katika maamuzi ili kuzuia athari za hasara ya maamuzi ya jazba:

Tusichotaka kutendewa tusiwatendee wengine

Kama hatupendi dini nyingine nje ya Ukristo isiingize udini katika utendaji wa Serikali, basi sisi wenyewe kama wakristo
tuhakikishe hatufanyi kosa lile lile dhidi ya dini nyingine. Hii ni kwa sababu tunataka kulinda haki ya uhuru na usawa kwa
kila dini kueneza imani yake pasipo upendeleo wala ubaguzi unaotokana na walioshika dola.

Mfano hai. Hivi majuzi yametokea malalamiko kwamba Rais kateuwa watu wa dini yake kushika nafasi nyingi za utawala.
Malalamiko hayo ndiyo kisa cha mimi kuanza kuandika makala haya. Takwimu zilipotolewa hadharani na kugundulika
kwamba bado idadi ya wakristo ni kubwa zaidi kuliko waumini wa dini nyingine, malalamiko juu ya udini yamekufa.

Kana kwamba hii haitoshi, ni hivi karibuni tu Rais kamaliza kuunda Serikali yake kwa kuteua Wakuu wa Wilaya. Takwimu
zinaonesha kwamba katika safu hii, idadi ya wakristo ni kubwa sana kuliko waumini wa dini nyingine! Swali langu la
uchokozi ni hili. Hivi kama idadi ya wakristo iliyopo sasa ingelikuwa wameteuliwa Waislamu, hali ingekuwaje? Bila shaka
yangetokea maandamano ya kupinga uteuzi huo.

Lakini sasa kwa kuwa ni watu wa dini yetu ndio wengi, tumenyamaza. Hivi kimya hiki hakiwezi kutafsiriwa na upande wa
pili kuwa na sisi tuna udini? Nina maana ya udini wa sisi kuendelea kuwa na watendaji wengi wa dini yetu dhidi ya dini
nyingine? Tunaweza kujitetea kwa hoja ipi na ikaleta mantiki? Ndiyo maana narejea kusema tena, tusichotaka
kutendewa sisi dhidi ya dini yetu, tusiwatendee watu wa dini  nyingine!

Apandacho mtu ndicho atakachovuna

Mfano wa kupanda mbegu ulitumiwa sana na Bwana Yesu katika kuwasilisha ujumbe wa mambo ya kiroho. Na sisi kama
wakristo tunatumia sana mithali za Yesu katika kuelimishana na kuonyana ili kuepuka madhara yawezayo kutupata kwa
sababu ya maamuzi na matendo yasiyo sahihi.

Katika hoja hii ningependa kusisitiza kwamba vitu hivi vya ‘madai dhidi ya…’, ‘malalamiko dhidi ya…’, au ‘tuhuma dhidi
ya…’ na yote yanayofanana na hayo ni sawa na ‘mbegu’. Kila madai yanayotoka upande mmoja wa dini dhidi ya upande
wa dini nyingine, hizo ni mbegu zinapandwa. Inawezekana wapandaji ama wanajua au hawajui matokeo ya mbegu
wanazopanda yatakuwaje huko baadaye; lakini hii haibadilishi ukweli kwamba wakati muafaka ukifika kila upande husika
utavuna kile walichopanda.

Badala ya kupanda mbegu za malalamiko au shutuma dhidi ya Serikali, hebu tupande mbegu za kuipongeza na kuitia
moyo kwa maneno na matendo. Huu ndio wajibu wa Kanisa kwa Serikali yoyote iliyoko madarakani. Kwa kusema hivi,
sina maana hata pale ambapo Serikali inafanya makosa yanayoweza kuleta mgawanyiko katika jamii iachiwe hivi hivi tu.
La hasha. Nafahamu kwamba nafasi ya Kanisa ni kuishauri Serikali. Na kama hekima na busara zikitumika vizuri wakati  
wa kutoa ushauri kwa Serikali, nina hakika matokeo yatakuwa ni mazuri. Kile kinachoogopwa kinaweza kuzuiliwa
kisitokee kabisa. Huku ndiko kupanda mbegu njema ambazo mavuno yake pia ni mema.

Kama nilivyowahi kudokeza huko nyuma kwamba katika jamii tunao watu wachache wenye hulka za kupenda
kusababisha shari miongoni mwa watu, ni busara tukawa na tahadhari ya kutokuwapa nafasi wakaendelea kupanda
mbegu za chuki na ubaguzi wa kidini, kwa kisingizio cha kutetea Ukristo. Tukiwaachia na kunyamaza kimya, wasio
wakristo watatafsiri kwamba wanaochochea uhasama wa kidini wanafanya hayo kwa niaba ya wakristo wote, wakati si
kweli kabisa.

Ukristo  hautetewi  kwa  maneno bali kwa nguvu za Roho Mtakatifu

Ninafahamu kwamba wale wote wenye hisia na hofu ya nchi kutoka katika misingi ya kidemokrasia na kuwa chini ya
Serikali ya kidini wanafikiri kwamba Ukristo umo  hatarini kufutwa. Aidha, historia ya Ukristo kufutwa barani Afrika,
hususan katika nchi za kaskazini ambazo hapo awali zilikuwa zinakaliwa na wakristo wengi, nako kunaongeza hofu ya
kujirudia kwa historia hiyo. Isitoshe, ninafahamu pia hali halisi inayoendelea huko Nigeria na Sudan, ambapo udini
unaendelea kusababisha mauaji kila iitwapo leo.
Hata hivyo, kama tukirejea katika maandiko na kuchunguza maana halisi ya Ukristo ulioandikwa katika Biblia,
tutagundua kwamba kamwe Ukristo halisi hauwezi kutetewa kwa maneno ya kisiasa hata kidogo. Ukristo unaye mtetezi
wake ambaye ni Roho Mtakatifu. Ushahidi tunaupata kwa Mtume Paulo jinsi alivyowaandikia Wakorintho akisema: “Neno
langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za
nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.” (1.Kor.4-5)

Kwa wale wasiofahamu historia ya watu wa Korintho ya enzi hizo, napenda kuwafahamisha kwamba mji wa Korintho
ulikuwa umejaa mahekalu ya dini yaliyojaa sanamu za miungu na mizimu ambapo nguvu za uchawi na mazingaombwe
vilikuwa vimetawala. Serikali za wakati huo zote zilikuwa zikiongozwa na kuendeshwa kwa sera za waganga na wachawi
wa enzi hizo.

Wakati Paulo alipoingia katika mji huu na kushuhudia nguvu za giza jinsi zilivyotawala, alitambua mara moja kwamba
hapa si mahali pa kuingiza ubingwa wa falsafa za kidini. Aligundua kwamba kinachohitaji kuingiza Ukristo ni kuidhihirisha
nguvu ya Kristo mwenyewe kwa ishara na miujiza itakayowafanya Wakorintho wajue kwamba yupo Mungu zaidi ya
miungu ambayo wamekuwa wakiiabudu miaka yote.

Ndiyo maana anawakumbusha Wakorintho wasisahau kwamba kilichowakomboa katika nguvu za giza hazikuwa hotuba
za kifalsafa, bali Injili yenye uweza wa Roho Mtakatifu hata wakaamua kujitoa katika ibada za sanamu na miungu,
wakamgeukia Kristo.

Ukristo wa Korintho ndio unahitajika sasa hapa nchini. Na Ukristo wa jinsi hii hatuwezi  kuutetea kwa maneno bali kwa
nguvu za Roho Mtakatifu. Kwa uzoefu wangu katika utumishi huu nimekutana na watu wa dini zote, wakristo kwa
waislamu na wa dini nyingine ambao wamekuja wakiwa wameteswa na kukandamizwa na nguvu za majini. Baada ya
kuwahubiria Injili yenye uweza na nguvu za Roho, mara majini yamewaacha huru na sasa wanafurahia matunda ya Injili
yenye mamlaka.

Hitimisho:

Manunguniko  kwamba Serikali ya awamu ya nne ina udini ni dhana potofu. Takwimu zimeonesha kinyume cha madai ya
dhana yenyewe. Hofu na hisia kwamba Ukristo katika Tanzania uko mashakani, haipaswi kutawala katika jamii ya Kikristo.


Aidha, tusisahau kwamba, nguvu ya kueneza Ukristo haimo katika mikakati ya kudhibiti maendeleo ya dini nyingine,
isipokuwa tunapaswa kuihubiri Injili yenye mamlaka kwa watu wa dini zote ili wafunguliwe kutoka katika matatizo sugu ya
kiafya, kifamilia, kiuchumi na kijamii.

Kuhubiri Injili ya mamlaka hakutegemei mazingira ya kisiasa yakoje. Upinzani dhidi ya Ukristo hautakomeshwa kwa
mikakati ya kisiasa. Wakati Injili ya mamlaka ikihubiriwa, Serikali iliyoko madarakani inahitaji dua, sala  na maombezi na
pale inalazimika kuishauri kwa hekima na busara  na kwa kupitia taratibu za ki-Katiba na kistaarabu.

                    
 Mwisho.
Jifunze na kusoma kwa makini maoni ya wengine