Mpango wa Yesu Kristo wa kumwondoa mtu
katika umaskini
Amini usiamini kichwa cha hoja hii kina maana hiyo hiyo unayoidhania kuwa ndiyo. Yaani, Yesu alikuja
duniani pamoja na mambo mengine ya kumwokoa binadamu na dhambi zake, pia alikuja na mpango wa
kufuta au kuondoa umaskini. Tatizo kubwa ni kwamba watu wengi hawajui ni aina gani ya umaskini ambao
Yesu alikuja kuuondoa, kwa kiwango gani na kanuni zipi za kukamilisha zoezi hilo. Hoja hii inakusudia
kuchambua kwa kina eneo hili kwa madhumuni ya kukuwezesha wewe msomaji kuijua kweli yote ambayo
matokeo yake ni kuwekwa huru kweli kweli:
Utangulizi
Ni hivi majuzi tu ambapo kwa neema ya Mungu nilipokuwa nikitafakari maandiko matakatifu, niligundua maandiko
yafuatayo: “Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu
yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema, amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa
kwao, na vipofu wapate kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” (Luka.4:
17-18)
Baada ya kusoma maandiko haya, macho yangu yalinasa kwenye maneno haya: ‘Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa
maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema’ . Maneno ya amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema
ndiyo yaliyonifanya hata mapigo ya moyo kubadilika ghafla, kana kwamba ndio nimekutana nayo kwa mara ya kwanza,
japokuwa nimeyasoma na kuyahubiri mara nyingi.
Kwanza nilijihoji ni maskini wa aina gani waliotajwa katika maandiko haya? Ni ‘maskini wa roho’ au ‘maskini wa kimwili’?
Kwa haraka haraka nikatafakari kwamba maskini wa roho’ ni yule mtu anayejiona ni mhitaji sana wa mambo ya Mungu
na anatafuta baraka za kiroho kutoka kwa Mungu.
Lakini niliposoma kwa makini nikagundua kwamba, vyovyote iwavyo, iwe ni ‘umaskini wa roho’ au ‘umaskini wa kimwili,’
bado ni ‘umaskini tu na mhusika hautaki katika maisha yake! Ndiyo maana maandiko yanaonesha kwamba Yesu
ametiwa mafuta na Roho ili kuwahubiri maskini habari njema.
Mara nilianza kujihoji binafsi kuhusu tafsiri ya maandiko haya. Nilianza kutafakari hivi ni ‘habari njema’ zipi ambazo mtu
maskini akizisikia zitaonekana ni njema kwake? Kitu kinachoitwa ‘Habari Njema’ kwa mhusika lazima kiwe ni ‘taarifa nzuri’
zenye kusababisha furaha na matumaini.
Kwa ufupi, nilibaini kwamba, kile maandiko yanacholenga ni kwamba Yesu Kristo alitiwa mafuta na Roho Mtakatifu ili
kuwaendea maskini na kuwapasha habari nzuri zinazolenga kuwaondoa katika umaskini wao! Nini? Ndiyo! Habari njema
kwa maskini ni taarifa zinazolenga kumwondoa katika umaskini wake!
Kuanzia hapo nikaanza kufanya utafiti upya wa maandiko unaoweza kuthibitisha kama vile nilivyoelewa ndivyo ilivyo
kweli kweli. Katika mfululizo wa hoja hii, nitaelezea kwa kina kuhusu mpango wa Yesu Kristo wa kumwondoa maskini
katika umaskini
Dhana kuu mbili potofu kuhusu
‘Injili ya utajirisho’ na ‘Injili ya umaskini’
Kabla sijaanza kuchambua jinsi Yesu alivyokuja duniani kumwondoa maskini katika umaskini wake, napenda niweke
bayana kuhusu dhana potofu ambazo zimekuwepo katika jamii ya Kikristo kuhusu tafsiri ya ‘utajiri’ na ‘umaskini’. Naweza
kusema kwamba zimekuwepo aina mbili za injili potofu, moja ni ‘Injili ya Utajirisho’ na ya pili ni ‘Injili ya Umaskini’!
Kabla sijaichambua ‘Injili ya Umaskini,’ hebu nitoe tafsiri ya aina mbili za umaskini. Biblia inaposema maskini mara nyingi
inalenga watu walemavu wa viungo ambao kwa ulemavu wao hawana uwezo wa kujipatia riziki kama binadamu wengine
wenye viungo kamili. Aina hii ya maskini hawa ndio ambao maandiko mengine katika Biblia yameagiza kwamba
wasaidiwe katika umaskini wao na wa kwamba kila amsaidiaye maskini ambaye ni mlemavu, atapata thawabu kubwa
kutoka kwa Mungu.
Aina ya pili ya umaskini ni ‘hali ya ufukara’. Mtu kushindwa kumudu kupata mahitaji ya lazima na muhimu kwa maisha
yake kwa sababu hana kipato cha kumwezesha kujikimu kimaisha. Huu pia unaitwa umaskini lakini ukweli lugha sahihi ni
‘ufukara’. Mara nyingi mtu ‘fukara’ si lazima awe mlemavu wa viungo. Anaweza kuwa ana viungo vyote kamili, lakini
akajikuta ni fukara. Baada ya tafsiri hii, hebu turejee katika ile dhana ya ‘Injili ya Umaskini’.
‘Injili ya Umaskini’ imebeba tafsiri kwamba, maisha ya umaskini ndio maisha bora ya utakatifu ambayo binadamu akitaka
kufika kwa Mwenyezi Mungu lazima ayaishi. Mifano kadhaa ambayo imekuwa ikinukuliwa ili kuhalalisha dhana hii ni
mfano wa Lazaro maskini na tajiri ambapo walipofariki dunia, maskini Lazaro aliingia peponi; na yule tajiri alijikuta kuzimu
mahali penye mateso makali. Kwa mfano huu imekuwa ikitafsiriwa kwamba walio maskini ndio wenye fursa ya kuingia
mbinguni kwa sababu tu ya umaskini wao?
Hivi ni kweli kwamba maskini wote wataingia mbinguni kwa sababu ya umaskini wao? Na ni sahihi kufikiri kwamba walio
matajiri watakwenda motoni kwa sababu ya utajiri wao? Kwa kifupi, niseme kwamba, wako maskini wengi sana
watakaojikuta katika moto wa Jehanamu ya moto na pia wako matajiri watakaoingia mbinguni pamoja na kwamba
walikuwa matajiri wa ulimwengu huu.
Haya, hebu turejee katika kuchambua dhana ya ‘Injili ya Utajirisho’. Mkazo wa dhana hii unadai kwamba kila mtu
anayemwamini Kristo, ‘lazima awe tajiri’. Na kama mwamini wa Kristo asipokuwa tajiri, basi bado anaishi chini ya laana na
huenda pia ni mtenda dhambi ndio maana bado ni maskini! Wenye kuhimiza ‘Injili ya Utajirisho,’ wamefikia kiwango cha
kuwaona wakristo ambao si matajiri kuwa ni watu ‘waliofungwa na nguvu za giza’ na wanahitaji kukombolewa katika
vifungo vya umaskini ili wawe matajiri. Pamoja na kwamba kuna ukweli kiasi kidogo katika madai haya, lakini tatizo kubwa
ni kule kuipitiliza mipaka ya maandiko kwa kupotosha watu kwamba utajiri ndicho kipimo cha ukamilifu wa imani ya
mkristo!
Mtazamo na mwelekeo wangu sikubaliani na dhana zote mbili. Mimi nina imani kwamba, wakati si mapenzi ya Mungu kwa
kila anayemwamini Kristo kuishi maisha ya ufukara; bado kuna mazingira ambayo mwamini atajikuta amepungukiwa
mahitaji yake kwa sababu ambazo ziko nje ya uwezo na uamuzi wake binafsi. Ndiyo maana nimeona ni bora nilete hoja
hii ya kuutafakari upya mpango wa Yesu Kristo wa kuondoa kumwondoa maskini katika umaskini wake. Naomba
nieleweke hapa. Kuna tofauti kati ya ‘mtu kuondoka katika umaskini’ na ‘umaskini kuondoka katika jamii’. Mimi
nazungumzia ‘mtu aliye ndani ya Kristo awezavyo kuondoka katika umaskini wake,’ hata kama ‘umaskini utaendelea
kuwepo katika jamii’.
Itaendelea toleo lijalo.
Jifunze na kusoma kwa makini maoni ya wengine
|