Taasisi ya ndoa na Sheria ya Ndoa Tanzania (9)
Mgogoro kati ya Waisraeli na Wapalestina ni
matokeo ya Ibrahim kuzaa na mjakazi

Na Mwassa Jingi
Katika matoleo matatu yaliyopita, tumeendelea kufuatilia maendeleo ya Taasisi ya Ndoa  kutokea kwenye
uzao wa watoto watatu wa Nuhu. Tayari tumeshaona vizazi vilivyotokana na watoto hawa na jinsi ambavyo
ulimwengu wa leo ulivyogawanyika kutokana na uzao huo. Leo tutaangalia baadhi ya madhara yaliyotokana
na Mzee Ibrahimu kuzaa na mjakazi Hajiri  na jinsi uzao huu unavyochangia katika mgogoro wa muda mrefu,
kati ya waarabu wa Palestina na  Waisraeli, ambao chanzo chake ni kuvurugwa kwa maadili ya ndoa.

Katika matoleo kadhaa ya mfululizo wa makala haya, nimeeleza jinsi Nuhu alivyomlaani mtoto wake Hamu, kwa sababu
aliona uchi wake wakati yeye Nuhu alipokuwa amelewa chakari na hajitambui. Kutokana na laana hiyo, basi uzao wote
wa Hamu ulibebeshwa laana na matokeo ya laana hiyo ni pamoja na uzao wa Hamu  kuendelea kuwa watumwa kwa
uzao wa  wale watoto wengine wawili wa Nuhu  yaani Shemu na Yafethi.

Pia tuliona, kutokana na historia ya uandishi wa Biblia kuwa uzao wa Shemu, ni pamoja na familia ya  Ibrahimu na
baadaye taifa lote la Israeli. Kwa upande wa Hamu, uzao wake uliendelea na kufikia kwa mataifa ya Waarabu na
Waafrika kwa ujumla wao, uzao ambao pia alitokea mjakazi wa Sara, yaani Hajiri, ambaye alitoka nchi ya Misri.

Ushahidi wa ukweli wa unabii huo wa Mzee Nuhu ni jinsi walivyo Waafrika na Waarabu ambao, ukiacha utumwa na
ukoloni uliokwishapita, lakini bado Waafrika na Waarabu wameendelea kuwa jamii duni  kifikra na kimaendeleo.

Huko nyuma nilishawahi kueleza kuwa Waafrika pamoja na kuwa na mali asili nyingi na hali ya hewa nzuri, lakini bado
vitu hivyo havijatusaidia kutengana na umaskini. Hata pale tunapopata misaada, bado misaada hiyo imeshindwa kuwa
chachu ya maendeleo yetu. Tutaendelea kutegemea uzao wa Shemu na Yafethi mpaka lini! Haijulikani.

Waisraeli ambao ni uzao wa Ibrahimu kupitia Isaka ni taifa dogo mpaka leo, lakini ni tishio kwa ulimwengu wote. Katika
nchi ambazo Waisraeli wamekuwepo, bado wameendelea kutamba katika nyanja zote za maendeleo, kuanzia elimu hadi
sayansi.Hata katika taifa kubwa kama Marekani, Wayahudi ndio moja ya jamii ambayo watu wake wanaishi maisha ya
juu. Na nchi  zingine ambazo zilikaribisha Waisraeli hazijawahi kujuta.
Laana kwa Hamu, haikuishia tu  katika kusababisha kero za utumwa na umaskini wa mwili, bali laana hizo zimeingia
mpaka kwenye misingi ya kiroho na kuleta madhara ya kiroho kwa binadamu.

Upinzani wa kidini  ni   matokeo ya uzao wa Ibrahimu na mjakazi.
Ukiacha dini ndogo ndogo  nyingi zilizoko duniani leo, bado utaona kuwa laana ya Hamu imekuja kuugawa ulimwengu
katika dini kuu mbili zinazopingana, yaani ukristo na Uislamu. Wakati ukristo umekuja kupitia kwa Wayahudi, Uislamu
ulianzia na uzao wa Hamu kwenda kwa Ishmaeli na hatimaye Mtume Muhammad. Mpaka sasa dunia inaendelea kuonja
madhara  mbalimbali katika maeneo yote ya kiroho, kimwili, kiuchumi na kiusalama, kutokana na kuwepo kwa familia ya
Ibrahimu katika mlengo wa kulia na kushoto.

Mbali na migogoro ya kidini na kiardhi, uzao wa Ishmaeli ambao umetokana na Hamu unaendelea kuongezeka na
kuimarisha uadui kati yake na uzao wa Shemu na Yafethi. Zaidi ya mtafaruku wa Mashariki ya Kati, kati ya Waisraeli na
Wapalestina, laana hiyo ya Hamu inajitanua zaidi kwa kuzaa Ugaidi( terrorism), ikiwa ni mbinu mpya ya uislamu
kupambana na ukristo kwa  kutaka kujiondoa na unyonge wa kutawaliwa kifikra zaidi.

Chuki kubwa iliyoko kati ya ulimwengu wa kiarabu ukiungwa mkono na ulimwengu wa kiislamu dhidi ya mataifa ya
Magharibi, mara nyingi huchukuliwa kuwa ni matokeo ya sera mbaya za nchi za Magharibi zikiongozwa na  Marekani,
lakini ukweli ni kwamba chuki hiyo chanzo chake ni uzao wa watoto wa Ibrahimu, yaani mtoto wa muungwana - Isaka na
mtoto wa  mjakazi - Ishmaeli.

Ni vema tupitie maandiko ya Biblia kwa  ufupi ili kutoa picha halisi ya hayo ambayo nimeyaeleza mpaka sasa.
“Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara
akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu,
mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo
lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, neno hili lisiwe baya
machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana
katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi  nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako”,
(Mwanzo 21:8-13). Maandiko haya yanatupa mitazamo tofauti kati ya Sara, Ibrahimu na Mungu.

Kusema kweli tangu mwanzo Ibrahimu alimpenda Ishmaeli mtoto wa mjakazi kama mtoto wake na wala hakutegemea
kuwa itatokea vinginevyo. Sara naye baada ya ile ahadi ya kumzaa Isaka kutimia, hakuona haja tena ya kuwa na
mjakazi wake pamoja na mtoto wake Ishmaeli. Kutokana na maandiko  hayo hapo juu, inaonesha kuwa kulikuwa
kutokupendana kwa watoto hao wawili, na hasa Ishmaeli kumchukia Isaka.

Kwa hiyo, Sara alimtaka mume wake Ibrahimu kumfukuza mjakazi na mtoto wake, kwa sababu ya kuona mtoto wake
Isaka anateswa na mtoto wa mjakazi na kwamba lile hitaji lake  la kutaka mtoto wa kurithi tayari halikuwepo kwa sababu  
Isaka tayari alishazaliwa.

Mzee Ibrahimu hata hivyo, hakuwa tayari kumfukuza mjakazi na mtoto wake, kwa sababu yeye alimhesabia Ishmaeli
sawa kabisa na Isaka. Yeye aliona kuwa wote, yaani Isaka na Ishmaeli  ni watoto wake na kwa hiyo hakuona sababu ya
kutenganishwa. Mungu aliamua kuingilia kati mjadala wa Ibrahimu na Sara na kumtaka Ibrahimu akubaliane na hoja ya
mke wake ya kuwafukuza Hajiri na mtoto wake. Kwa hiyo Ibrahimu alikubaliana na hoja ya mke wake na hivyo
akamfukuza mjakazi wake na mtoto.

Kwa nini Mungu awatenganishe Isaka na Ishmaeli?
Hili ni swali la msingi, ingawa ni swali gumu. Kwa akili ya kibinadamu, tusingetegemea Mungu akubaliane na hoja ya
Sara, ya kutaka mjakazi wake pamoja na mtoto wafukuzwe. Tena baya zaidi ni kwamba walifukuzwa wakiwa hawajui pa
kwenda, tena katika mazingira magumu ya jangwa. Kwa nini Mungu  ambaye ni mwenye huruma na upendo akubaliane
na hoja ya kufukuzwa kwa Hajiri na mtoto wake? Bila shaka, Mungu alijua tatizo ambalo lingetokea siku za mbeleni.
Aidha, kwa upande mwingine tunaweza kuchukulia tu kwamba ule ulikuwa ni  wivu Sara  kutaka mtoto wake tu ndiye
arithi.

Kama Ishmaeli akiwa bado mtoto mdogo tayari alishaanza kumchukia mdogo wake Isaka, je hali ingekuwaje kama wote
wawili wangeendelea kukua pamoja  kama familia moja ya Mzee Ibrahimu? Kwa vyo vyote vile lazima kungekuja kuwa na
tatizo kubwa kuliko hata lile la kufukuzwa kwa Hajiri na mtoto wake. Inawezekana hata lile lililotokea kwa familia ya
Adamu, ambapo Kaini alimuua ndugu yake lingetokea.   

Lakini tukirejea nyuma utakumbuka kuwa Mungu alimwambia Ibrahimu kuwa mrithi wake angetokana na yeye na mkewe
Sara. Kama Isaka na Ishmaeli wangekua pamoja, ilikuwa pia lazima wote wawili warithi pamoja. Na pili jina la Ibrahimu
lingeendelezwa kutokana na uzao wa Isaka na Ishmaeli na hivyo kuchanganyika kwa uzao wa Hamu na Shemu kinyume
na maagizo ya laana ya Mzee Nuhu.  Ingawa Ibrahimu alishasahau hiyo, Mungu hakusahau.

Swali lingine ambalo tunaweza kujiuliza nalo ni hili; kuna dhambi gani au kosa gani mtoto wa Sara (muungwana) kurithi
pamoja na mtoto wa mjakazi?
Kimsingi, hoja ya kuwa mtoto wa muungwana hatarithi na mtoto wa mjakazi ilitoka kwa Sara ingawa ilikuwa na msingi wa
kiroho pia na ndiyo maana  Mungu naye akaiunga mkono. Je, Mungu ana  ubaguzi?

Hii ndiyo hoja kubwa miongoni mwa jamii ya kimataifa kuhusu mgogoro kati ya Wapalestina na Waisraeli, ambapo karibu
dunia yote wanaona kuwa sio kweli kuwa  Mungu kwa namna moja au nyingine ahusike na ubaguzi unaoendelezwa na
wayahudi na wapalestina leo, ikiwa na maana kuwa    baadhi ya watu kama wayahudi, Mungu awape  upendeleo
maalumu tofauti na tabia yake kuwa yeye si Mungu wa upendeleo.

Ni kweli Mungu hana upendeleo, isipokuwa, mwanadamu ndiye anayechagua mwelekeo wake wa baadaye, kutokana na
hiari yake ya kutumia akili na kufanya maamuzi. Uchaguzi wa mwanadamu katika njia zake ndio unaoweza kumfanya
Mungu aonekane ni mbaguzi. Huko nyuma tumeona kuwa Mungu alikubaliana na laana ya Nuhu kwa mtoto wake,
vinginevyo hiyo laana isingempata Hamu. Lakini Mungu aliidhinisha laana hiyo kwa sababu ya kitendo cha Hamu,
ambacho kilikuwa kinyume cha maadili.

Kama Mungu angeruhusu mtoto wa mjakazi arithi pamoja na mtoto wa muungwana (Isaka), basi ingekuwa
anaunganisha tena uzao wa watoto wa Nuhu kuwa na mazingira yanayofanana. Hiyo nayo bila shaka ingesababisha
madhara makubwa kwa kizazi cha binadamu mapema zaidi kuliko ilivyotokea kwa Isaka na Ishmaeli.

Mungu alichofanya ni kuchukua hatua ya makusudi za kumsaidia Hajiri amlee mtoto wake, na yeye kuahidi kuwa
Ishmaeli naye angekuwa taifa kubwa. Mpaka leo vizazi vya Isaka na Ishmaeli ndivyo vinavyougawa ulimwengu wa leo
katika fikra na mtazamo tofauti tofauti kidini na kisiasa. Ulimwengu wa uzao wa Ishmaeli umeendelea kukua kidini na
kisiasa, ukishindana na ule ulimwengu uliotokana na watoto wale wengine wawili wa Mzee Nuhu.

Mbali na laana ya Hamu, ambayo iliuweka uzao wake chini ya utumwa, bado uzazi wa Ibrahimu na mjakazi wake nao
uliendeleza kuifanya hali iwe mbaya zaidi, sio tu kuwa na watu bora (superior) na duni (inferior), lakini hali hiyo
imeongeza uadui kati ya uzao wa Isaka na Ishmaeli, kama ambavyo mgogoro wa Mashariki ya kati ulivyo. Mgogoro huo
una sura zote mbili, kisiasa na kidini.

Mtume Paulo naye amejaribu , kwa neema ya Mungu, kuchambua sababu za mtoto wa mjakazi kutokurithi pamoja na  
mtoto wa muungwana. Hivyo ndivyo anavyosema. “Kwa maana imeandikwa ya kuwa, Ibrahimu alikuwa na wana wawili,
mmoja kwa mjakazi, na mmoja  kwa muungwana. Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa muungwana kwa
ahadi. Mambo haya husemwa kwa mfano; kwa maana hawa ndio kama maagano mawili, moja kutoka mlima Sinai, lizaalo
kwa utumwa, ambalo ni Hajiri. Maana Hajiri ni kama mlima Sinai ulioko Arabuni, umelingana na Yerusalemu wa sasa;
kwa kuwa anatumika pamoja na watoto. Bali Yerusalemu wa juu ni muungwana, naye ndiye mama yetu sisi…..Basi,
ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi. Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwuudhi yule
aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa. Lakini linasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana
mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa muungwana.  Ndiposa, ndugu zangu, sisi sio watoto wa
mjakazi, bali tu watoto wa huyo aliye muungwana (Wagalatia 4:21-31).

Ni kutokana na uzazi wa muungwana, yaani Sara mke wa Ibrahimu ndio ulimwengu ulikuja kupata mkombozi,Yesu Kristo.
Tunajifunza nini na nadharia hii ya mtoto wa muungwana na mtoto wa mjakazi au mtumwa? Nadharia hii ina uhusiano
mkubwa na maendeleo ya Taasisi ya Ndoa na kizazi cha binadamu. Pale ambapo wanadamu wanaishi na kuzaliana kwa
kufuata misingi ya ndoa kama ilivyowekwa na Mungu, basi uhusiano wa Mungu na kizazi hicho huwa mzuri na
maendeleo ya binadamu huendelea kupata kibali kwa Mungu. Mazingira ya ndoa yana mchango chanya au hasi katika
maendeleo ya kimwili au kiroho, kwa binadamu kutegemeana na ubora wa ndoa yenyewe, kama inafuata misingi sahihi
au la.
MAKALA ILIYOPITA YA 8