| Taasisi ya Ndoa na Sheria ya Ndoa Tanzania (10) Mwendelezo wa ndoa katika kizazi cha Ibrahimu Katika matoleo kadhaa yaliyopita ya makala haya, tumekuwa tukifuatilia uendelezwaji wa misingi halisi ya ndoa kama ilivyowekwa na Bwana Mungu mwenyezi. Na msingi mkubwa ambao kila mwanadamu anapaswa kuuangalia na kuuheshimu ni ule wa “mume mmoja kwa mke mmoja”. Huko nyuma tuliona kuwa uzao ambao ulikiuka msingi huu ni ule ambao ulimwasi Mungu.Uzao ambao ulizingatia misingi ya ndoa, Mungu aliendeleza uhusiano na kizazi hicho. Tumeona pia kwamba kuyumba kwa familia ya Ibrahimu kulisababishwa na familia hiyo kuamua kupata mtoto kupitia mjakazi wao na madhara ya kuzaliwa kwa Ishmaeli yapo mpaka leo, yaani uadui kati ya wayahudi na wapalestina. Mambo hayo kwa ufupi yanatuonesha madhara ya kukiuka misingi ya ndoa. Hata leo hii madhara yanayozikumba familia nyingi katika dunia hii kwa kiasi kikubwa hutokana na kuishi kinyume na matakwa ya misingi ya ndoa. Tuangalie ndoa ya Isaka Kabla ya Mzee Ibrahimu kufariki dunia, aliona ni vema mtoto wake wa pekee aliyempata kwa muujiza Isaka aendeleze uzao sahihi kwa kupata mke sahihi kutoka kwa familia bora. Tunasoma hivi:”Basi Ibrahimu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, na Bwana alikuwa amembariki Ibrahimu katika vitu vyote. Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba, aliyetawala vitu vyake vyote…………. Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, nami nitakuapisha kwa Bwana Mungu wa mbingu na Mungu wa nchi kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za wakanaani ambao nakaa kati yao, bali enenda hata nchi yangu, ukamtwalie mwanangu mke (Mwanzo 24:1-4). Ibrahimu kama tunavyojua aliondolewa katika familia yake na kuambiwa aende katika nchi ambayo ni ya ukoo wa Hamu, yaani uzao wa mtoto wa Hamu aliyeitwa Kanaani, na watu waliotokana naye waliitwa wakaanani. Kwa kufuatilia ukoo wa watoto watatu wa Nuhu, bado Ibrahimu na wakanaani walikuwa karibu tu kama ndugu. Lakini kwa nini hakutaka mtoto wake apate mke kutoka kwa watu aliokuwa anaishi nao, yaani wakanaani ambao walitokana na kizazi cha Hamu? Ibrahimu alijua fika kuwa hao hawakuwa watu sahihi kwa kutwaa mke sahihi. Mzee Ibrahimu kwa kujua ulazima wa ndoa sahihi kwa maendeleo ya kizazi cha mtoto wake, hakulichukulia suala la mtoto wake Isaka kupata mke kwa mizaha. Ibrahimu pamoja na uzee wake huo bado aliendelea kumheshimu Mungu kama ilivyokuwa wakati mwingine wowote. Na kutokana na uchaji Mungu wake, pia alitambua umuhimu wa mchango wake kwa ndoa ya mtoto wake Isaka, kabla ya kufa kwake. Alijua kuwa mke mwema hupatikana katika familia inayomjua Mungu. Mzee Ibrahimu alijua ulazima wa mtoto wake kupata mke kutoka kwa familia aliyokuwa anaijua, ingawa hakumfahamu yule binti ambaye angekubali kuwa mke wa mwanawe Isaka. Ili kuhakikisha mtumishi wake hafanyi kinyume na maagizo yake, Mzee Ibrahimu aliamua kumwapisha mtumishi wake kwa Mungu ili mtumishi huyo akivunja kiapo hicho apate madhara yeye mwenyewe. Kule kumwapisha mtumishi wake kunaonesha ni kwa kiasi gani Mzee Ibrahimu alijua umuhimu wa mtoto wake kupata mke sahihi. Kwa wale waliobahatika kusoma makala niliyoandika kuhusu “Ulimwengu wa wasioolewa” iliyotoka katika ukurasa huu mwaka jana, bila shaka watakumbuka jinsi nilivyotumia sura hii ya 24 ya kitabu cha Mwanzo kuainisha kanuni nne za lazima kwa watu wanaotaka kuingia kwenye ndoa kuzifuata. Ninachotaka kueleza hapa kwa ufupi ni kwamba historia hii ya watu wa Biblia -Ibrahimu na Isaka inatuonesha jinsi watu hao walivyofuata misingi ya ndoa, na kwa kufanya hivyo vizazi vyao viliendelea vema kwa kudumisha uhusiano wao na Mungu, hatua ambayo ilisaidia pia kwa ustawi wa maisha yao kimwili na kijamii. Ndoa ni kiini cha familia na taifa bora, ndiyo maana tunasisitiza kufuatwa kwa kanuni na misingi yake kikamilifu. Tunaona kuwa mtumishi wa Mzee Ibrahimu alifuata maagizo ya bwana wake na kufanikiwa kupata mke mwema kwa ajili ya Isaka. Mungu alivyolinda ndoa za Ibrahimu na Isaka Ndoa kati ya Ibrahimu na Isaka zilipata baraka na ulinzi kamili wa Mungu, hata pale kulipokuwa na tishio la kuzivunja kutoka nje. Ukisoma sura za ishirini na ishirini na saba za kitabu cha Mwanzo, utaona jinsi ambavyo Ibrahimu na Isaka walivyokutana na matishio ya kunyang’anywa wake zao na Mfalme Abimeleki kwa nyakati tofauti. Ingawa wao wenyewe hawakuwa na uwezo wa kuwalinda wake zao katika mazingira magumu ya njaa wakiwa ugenini, lakini Mungu aliweza kuwatetea na kuwalinda wake zao wasiporwe na watu wengine pale ambapo wao (Ibrahimu na Isaka), walikuwa tayari kuwaachia ili wasiuawe na Mfalme Abimeleki au watu wengine ambao wangetamani wake zao. Biblia inasema Sara na Rebeka walikuwa ni wanawake wazuri wa uso na kwa hiyo watu wengine na hasa wafalme wangeweza kuwanyang’anya au kuwaua wao ili wawapate wake zao. Hii ndio faida kubwa ya kuwa na uhusiano na Mungu, kwani Mungu anakuwa mhusika namba moja katika kuzuia ndoa kusambaratika pale ambapo familia inaweza kupitia mikikimikiki ya maisha. Je! Hali ingekuwaje kama Ibrahimu na Isaka wasingefuata maadili na misingi ya Mungu katika kujenga ndoa zao? Bila shaka yoyote Mungu asingehusika kabisa katika ulinzi wa wake zao na familia zao kwa ujumla. Ingawa Ibrahimu na Sara, Isaka na Rebeka hawakupata watoto wengi katika ndoa zao, lakini polepole Mungu aliendeleza vizazi vyao na hatimaye kuwa taifa na mataifa kama Mungu alivyomwapia Ibrahimu tangu mwanzo. Ingawa maisha ya Ibrahimu yanaonekana kuwa ya matatizo kindoa, lakini kusudi la Mungu lilitimia. Kama Ibrahimu babaye, hata uzao wa Isaka nao ulikuwa wa matatizo. Mke wa Isaka, Rebeka naye kama mama mkwe wake, alikuwa tasa. Bado hali hiyo haikumwondoa Isaka katika kumtumaini Mungu. Isaka kwa sababu alimjua Mungu, alimwomba Mungu ampe uzao. “Isaka akamwomba Bwana kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye Bwana akamwitikia na Rebeka mkewe akachukua mimba, (Mwanzo 25:21). Uhusiano mzuri kati ya mtu na Mungu utamsaidia katika mambo mengi, ikiwa ni pamoja na yale ambayo hayawezekaniki kwa uwezo wa kibinadamu. Isaka hakufikia kutafuta ufumbuzi nje ya mapenzi ya Mungu. Kwa mtu mwingine asiyemjua Mungu, kutokupata mtoto ni jaribu tosha la kumwondoa katika imani. Lakini tunaona Isaka alipoona mke wake hazai hakufikiria kuoa mke mwingine, bali alimwomba Mungu na Mungu alimwitikia. Huku ndiko kuendeleza misingi ya ndoa, kwa sababu ndoa ni taasisi aliyoianzisha Mungu, ataendelea siku zote kuhakikisha kuwa wale wote wanaoiheshimu na kuifuata misingi ya ndoa, maisha yao yanafanikiwa, ikiwa ni pamoja na kuendelea kupata uzazi halali. Kumbuka ni Mungu ndiye aliyesema watu wazae na kuongezeka. Je, ataachaje kuhusika na masuala ya ndoa na familia, wakati ndiye aliyeanzisha familia na ndoa ya kwanza? Mungu anaheshimu ndoa kuliko watu wanavyofikiria. Kama wanadamu wataendelea kumtii Mungu katika kufuata misingi ya ndoa, Mungu naye ataendelea kuwasikia, hata pale matatizo yanapojitokeza katika ndoa na familia zao. Siku hizi, na hasa vijana hawana tena imani kwa Mungu kuhusu maisha ya ndoa na familia. Vijana wa leo hudiriki hata kufikiria kuwa na mahusiano ya kindoa (kufanya ngono), kabla ya ndoa kwa sababu tu za kibinadamu, na moja ya sababu kubwa ikiwa ni kupima uwezekano wa mwanamke kuzaa. Katika makanisa mengi ya kidini, ndoa nyingi hufungwa kanisani, watu wakiwa tayari wameshakuwa familia kwa kuishi pamoja, wengine huwa tayari ni wajawazito wakati wa kufunga ndoa. Hii kwa vijana huwa ndio ushahidi wa kile wanachofikiria kuwa ni vema kujua kama mke ana uwezo wa kuzaa au hapana, kabla ya kuingia kwenye mkataba wa ndoa. Mchezo huu, ingawa unaweza kuonekana kuwa una mantiki kibinadamu, lakini upo nje ya misingi ya ndoa. Isaka aliletewa mke na wala hakuletewa yule mke kwa majaribio. Kama Isaka angekuwa na akili kama za vijana wa leo, maana yake angemrudisha Rebeka kwao pale alipochelewa kuzaa. Isaka kwa sababu alipata mke kwa taratibu zote halali na za ki-Mungu, hakuwa na shaka yoyote hata alipogundua kuwa mke wake ni tasa. Alijua utasa huo ni tatizo dogo kwa Mungu, kwa sababu ni Mungu ndiye aliyehusika katika kumpatia huyo mke. Kama taratibu zilizotumika kumpatia Isaka mke hazikumhusisha Mungu, Isaka asingekuwa na ujasiri hata wa kumkaribia Mungu, pindi mke wake alipoonekana kuwa tasa. Lakini kwa sababu alikuwa na uhakika kuwa huyo mke amempata kwa njia na taratibu halali, ndio maana alikuwa na ujasiri wa kumwomba Mungu aingilie kati na kuvunja utasa wa mke wake. Angalizo kwa vijana Ni vema vijana wetu wa leo na hasa wale waliokwisha kutoa maisha yao kwa Yesu Kristo, kutokuwa na wasiwasi wowote katika kufikiria maendeleo ya familia na hasa suala la kupata au kutokupata watoto baada ya ndoa. Maisha ya Ibrahimu na mwanawe Isaka yanatosha kabisa kuwa ushahidi na kielelezo kuwa maisha ya ndoa yapo mikononi mwa Mungu, kwa sababu yeye Mungu ndiye mwanzilishi wa Taasisi ya Ndoa. Jambo la msingi kwa kila kijana wa kiume kuzingatia ni kufuata misingi, kanuni na taratibu zilizoainishwa katika Biblia wakati wa kutafuta mke. Mara baada ya kupata mke kwa kufuata taratibu zote za ki-Mungu, hakuna tena sababu yoyote ya kuwa na shaka juu ya uzazi wa mke wako. Kama mazingira au matatizo ya kuchelewa kupata mtoto kama ilivyotokea kwa Ibrahimu na Isaka yatatokea, basi Mungu yule wa Ibrahimu na Isaka ndiye Mungu wako leo na kwa kiwango kile alichowasaidia Ibrahimu na Isaka kuondoa matatizo ya familia zao, ndivyo atakavyofanya hata kwako leo. Mungu habadiliki na ahadi zake ni za kweli. Kila anayemtumaini hatatahayarika. |
| Jisomee makala ili uelimike na kupanua ufahamu |