Taasisi ya Ndoa na Sheria ya Ndoa Tanzania (12)
Mwanaume hawezi kupenda wake wawili bila upendeleo
Katika toleo la juma lililopita, tuliona jinsi familia ya Yakobo ilivyoongezeka kwa kasi kutokana na uzao wa
wake zake wawili na pia uzao wa wajakazi wao. Tuliona pia kwamba, Yakobo alioa wake wawili, yaani Lea na
Raheli, sio kwa mapenzi yake, bali kwa kulazimishwa kumuoa Lea ambaye hakuwa chaguo lake. Ingawa
wake zake Yakobo walikuwa ni mtu na mdogo wake, lakini waliishi bila kupendana katika maisha yao yote.
Leo tunaendelea na kuangalia mwendelezo wa chuki ya wake zake Yakobo kwa watoto na mwelekeo mzima
wa kizazi cha Mzee Yakobo, ambaye kwa jina lingine alijulikana kama Israeli.
Yesu alipokuwa anafundisha juu ya kanuni muhimu za maisha alisema maneno yafuatayo: “Hakuna mtu awezaye
kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda yule; ama atashikamana na huyu, na
kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali”,(Mathayo 6:24).
Kanuni hii ya kutumikia mabwana wawili ina mfanano wa pekee, hata kwa maisha ya ndoa na hasa tunapoangalia kisa
cha Yakobo kuoa wake wawili.. tuliona jinsi ambavyo Yakobo hakuweza kuwapenda wake zake wawili. Yeye Yakobo
tangu mwanzo alimpenda Raheli. Ilipotokea kuwa amepewa Lea badala ya Raheli, bado pendo lake kwa Raheli
liliendelea na alivumilia hata miaka mingine saba akimtumikia Labani ili ampate Raheli. Na bila shaka Labani aliweka
kikwazo hicho cha miaka saba kwa Yakobo ili kumkatisha tamaa asiendelee na madai yake ya kumtaka Raheli na
badala yake aridhike na mke wake Lea.
Kwa sababu moyo wa Yakobo ulishampenda sana Raheli, alikuwa tayari kwa lolote ili mradi ampate Raheli. Hii ndio siri
ya kupenda. Mtu akishapenda yuko tayari hata kufa kwa mke au mpenzi wake. Isitoshe pamoja na Yakobo kujitahidi
kwa akili za kawaida kuwatendea sawa wake zake ambao aliwapata kimazingira, bado wake hao ambao walikuwa mtu
na mdogo wake hawakuweza wao wenyewe kupendana. Lea aliona kuwa yeye ana sababu ya kumchukia Raheli kwa
sababu alimnyang’anya mume wake. Raheli naye, alikuwa na kiburi kwa sababu alijua kuwa tangu mwanzo yeye ndiye
aliyekuwa chaguo na kipenzi cha Yakobo. Raheli alijua fika kuwa dada yake Lea hakuwa anapendwa na Yakobo, bali
aliozwa kwa ujanja kwa Yakobo na baba yao Labani.
Ni dhahiri kuwa Yakobo hakuwahi kumpenda Lea hata kama aliendelea kuitwa mke wake; ni mke aliyepewa na Labani
na halikuwa chaguo lake tangu mwanzo. Na Yakobo kwa sababu alimpenda sana Raheli, asingeweza kumwacha Lea
kwa sababu hiyo peke yake ingekuwa sababu tosha ya Labani kumnyima Yakobo hata ile fursa ya kumpata Raheli.
Kule Yakobo kuvumilia kuwa na Lea ingawa alikuwa hampendi, kulimsadia kumshawishi Mzee Labani kumruhusu
amwoe mdogo wake Lea, yaani Raheli baadaye.
Na ni dhahiri pia kuwa Yakobo aliendelea kumpendeza sana Raheli, hata kama alikuwa tasa. Huu ni ushahidi mwingine
kuwa ndoa halisi na ya kweli ni ile ambayo msingi wake mkuu ni upendo. Kimsingi, mwanadamu anatakiwa kumpenda
mwanamke mmoja katika maisha yake yote na ikitokea akaanza kupenda mwanamke au wanawake wengine, maana
yake, tayari huyu mwanaume ameshaanza kumchukia yule mke wake wa kwanza. Kibaya zaidi ni kwamba hakuna
mwanaume ataweza kuwapenda wake zake wawili au zaidi, ingawa kwa mdomo anaweza kudai hivyo, lakini moyoni
mwake lazima anampenda mmoja zaidi; na kama alivyosema Yesu kuwa hakuna mtu anayeweza kutumikia mabwana
wawili, vivyo hivyo hakuna mwanaume anayeweza kuwapenda wake wawili, ama atampenda huyu na kumchukia
mwingine na chuki hiyo hupandwa hata ndani ya watoto wanaotokana na familia hiyo.
Kwa upande wa wanawake, wao ndio zaidi. Hakuna mwanamke ambaye yuko tayari kuchangia mume na mke
mwingine. Nimewahi kuongea na wanawake wengi, hata wale ambao dini zao zinaruhusu waume wao kuoa wake zaidi
ya mmoja, nao hawakubaliani kabisa na mchezo wa kuchangia mume na mke mwingine. Wanawake wanaoolewa ndani
ya ndoa nyingine au wanapoletewa mke mwenza huwa hawana uchaguzi, kwa sababu nyingine za kijamii na kiuchumi,
lakini si kwa sababu ya mapenzi yao. Hata wale wanaokubali kuolewa ndani ya uke wenza, huwa na mawazo kuwa wao
ndio wamependwa zaidi na kwa hiyo yule mke wa zamani hatakuwa na maana tena kwa mwanaume.
Ndoa za wake wengi huendeleza chuki ndani ya familia
Tumeona jinsi familia ya Yakobo ilivyoendelea kuongezeka kwa kasi lakini bila upendo ndani yake. Lea aliendelea
kumchukia mke mwenza Raheli maisha yake yote. Biblia inasema anayemchukia ndugu yake ni sawa na muuaji,
(IYohana 3:15). Wake zake Yakobo walishindana kuzaa ili kumfanya Yakobo ampende mmoja wao na kumchukia
mwingine.
Kwa mtazamo huo ni kwamba mwanaume anapoamua kuoa wake wengi, maana yake analeta chuki ndani ya familia
yake na mke mmoja anapokuwa anamchukia mwenzake, ndio kusema anahesabiwa kuwa muuaji. Chuki tangu
mwanzo husababisha mauti. Kaini alipomchukia mdogo wake Habili, mwisho alichukua hatua ya kumuua. Esau
alipopokonywa haki ya mzaliwa wa kwanza, aliazimia kumuua mdogo wake Yakobo. Na Kwa sababu chuki ni chanzo
cha vifo vingi, haipaswi kabisa wanadamu kujitakia hali hiyo ya chuki kwa njia ya ndoa ya wake wengi.
Chuki inayotokana na wake kuchukiana kwa sababu ya kumchukia mwenzake huhamia pia kwa watoto. Mungu ni
mwenye huruma, pamoja na chuki iliyokuwepo ndani ya familia ya Yakobo na hasa Lea kwa Raheli, Mungu bado
alisikia kilio cha Raheli cha kutaka mtoto. Kiu ya Raheli kupata mtoto haikuishia kwa kuwa na watoto wa mjakazi wake
Bilha. Raheli aliendelea kumlilia Mungu mpaka Mungu akanyosha mikono na akamfungua tumbo lake na hivyo Raheli
alipata mtoto na kumwita Yusufu. Yusufu ndiye aliyekuwa mtoto wa kwanza wa Raheli kwa kujifungua mwenyewe,
ukiacha wale ambao aliwapata kupitia mjakazi wake Bilha.
Mateso ya Yusufu ni matokeo ya chuki ya wake zake Yakobo
Kwa wasomaji wa Biblia, kisa na historia ya Yusufu inajulikana vizuri.Tafsiri rahisi ambayo wasomaji wengi wa Biblia
wanayo kuhusu maisha ya Yusufu ni ile ya kuchukiwa na ndugu zake kwa sababu baba yake alimpenda na
kumpendelea sana kuliko watoto wengine. Ni kweli Mzee Yakobo alimpenda sana mtoto wake Yusufu, na hivyo Yusufu
akachukiwa na ndugu zake wakubwa ambao wengi wao walikuwa ni watoto wa Lea.
Lakini Mzee Yakobo alikuwa na sababu nyingi za kibinadamu za kumpenda Yusufu kuliko watoto wengine. Kwanza ni
lazima tukumbuke kuwa Yakobo alimpenda sana Raheli tangu mwanzo, na alimsotea kwa miaka 14 kwa maana alitumia
miaka saba ya kwanza, lakini badala ya Raheli alipewa Lea. Alisota miaka mingine saba na hatimaye akampata Raheli,
kipenzi chake cha moyo.
Isitoshe, bado pendo la Yakobo kwa Raheli halikuchuja hata pale Raheli aliposhindwa kupata watoto kwa sababu ya
utasa. Kwa akili za kawaida ni rahisi kufahamu kwa nini Yakobo alimpenda sana Yusufu kuliko watoto wake wengine.
Kama Yakobo alimpenda sana Raheli, kitendo cha Raheli kuchelewa kupata mtoto halikuwa tatizo tu kwa Raheli bali
hata kwa mumewe Yakobo.
Bila shaka yoyote, Yakobo alishiriki adha ya mke wake Raheli kutokana na kutokupata mtoto kwa muda mrefu.
Kuzaliwa kwa Yusufu sio tu ilikuwa ni furaha na faraja kwa Raheli, bali kwa Yakobo pia. Hii ndiyo sababu ya msingi ya
Yakobo kumpenda mtoto wake Yusufu kuliko watoto wengine, ingawa kumpenda huko kulisababisha kuchukiwa kwa
Yusufu na ndugu zake wengine.
Lakini hayo yote, tisa, kumi ni sababu ya chuki hii kwa Yusufu. Ni dhahiri kama Yakobo angeoa mke mmoja tu Raheli
kama ilivyokuwa chaguo lake tangu mwanzo, hali ya chuki iliyokuja kuigubika familia ya Yakobo na kisha chuki hiyo
kuhamia kwa Yusufu isingekuwepo.
Ndoa ya wake wengi haikuwa mpango wa Mungu tangu zamani
Huko nyuma tuliona kuwa chuki ndani ya familia ya Mzee Ibrahimu ililetwa na uamuzi wa familia hiyo kuamua kupata
mtoto kupitia mjakazi wao. Chuki hiyo imeendelea mpaka leo na matokeo yake ni vita visivyo isha kati ya Waarabu na
Waisraeli. Chuki kutawala familia ya Yakobo ni ushahidi mwingine kuwa ndoa ya wake wengi sio mpango wa Mungu.
Chuki ndani ya familia ya Yakobo ilitokana na aina ya ndoa aliyokuwa nayo Yakobo. Kama ilivyo kawaida kwa kanuni
ya asili kuwa chuki huzaa mauti,ndivyo hali hiyo ilivyokuja kujirudia kwa familia ya Yakobo kama ilivyokuwa kwa familia
ya Adamu na Hawa na ya Isaka na Rebeka. Watoto wa Yakobo, ndugu zake Yusufu, baada ya kuendelea kumchukia
Yusufu kwa muda mrefu, hatimaye waliazimia kumuua kabisa ili asiendelee kuwa kero kwao.
“Basi Israeli (Yakobo) akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu
ndefu. Ndugu zake wote wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani” ( Mwanzo 37:3,4). “Wakamwona
toka mbali na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamuue”, (Mwanzo 37:18).
Kwa bahati mbaya, maskini Yusufu hakujua kama ndugu zake wakubwa walikuwa wanamchukia; na bila shaka hata
baba yao hakujua jinsi ambavyo Yusufu alikuwa chukizo kwa ndugu zake, kwa kisingizio kuwa alikuwa anapendwa na
baba yao kuliko wao. Na kwa sababu Yusufu hakujua kuwa alikuwa anachukiwa na ndugu zake, aliendelea kutoa siri
ya ndoto zake kwao. Hii iliongeza chuki zaidi na ndugu zake wakakata shauri la kumuua. Mlolongo wa chuki hii shina
lake ni aina ya ndoa aliyokuwa nayo Mzee Yakobo, yaani ndoa ya wake wengi.
Mungu alipoweka misingi ya ndoa ya mume mmoja kwa mke mmoja, alijua kuwa penzi la ndoa lisipoheshimiwa kwa
kufuata msingi huo, basi madhara yake ni kama hayo ambayo, familia ya Mzee Yakobo ilikumbana nayo. Kutokana na
hali halisi ya wakati huo, wakati ambao jamii hiyo haikuishi chini ya sheria yoyote, basi rehema za Mungu zilifanya kazi
kwa namna ya pekee. Mungu aliendelea kuheshimu agano lake na Ibrahimu kwa kuendeleza kizazi cha Yakobo
pamoja na kizazi hicho kuishi chini ya mazingira ya chuki.
Yusufu aliendeleza agano la Mungu na Ibrahimu
Mungu alimwahidia Ibrahimu kuwa angembariki na kuufanya uzao wake kuwa taifa kubwa. Ni kweli tangu Ibrahimu na
Isaka hapakuwepo na ongezeko kubwa la familia kama ile ya Yakobo, ambayo iliongezeka kwa kasi kutokana na
mashindano ya kuzaa kati ya wake zake wawili wakitumia na wajakazi wao. Mungu kwa kuheshimu mapenzi sahihi ya
Yakobo tangu mwanzo kwa kumpenda Raheli awe mke wake, alisikia maombi ya Raheli na akamfungua utasa wake.
Zaidi ya yote, baraka za Mungu kwa Ibrahimu ziliendelezwa katika familia ya Yakobo kwa kupitia Yusufu ambaye
alikuja kuwa hifadhi ya familia yote ya Yakobo nchini Misri.
Ingawa ndugu zake kwa chuki waliamua kuachana na Yusufu, lakini hiyo haikusitisha ahadi ya Mungu kwa Ibrahimu ya
kumbariki na kumfanya kuwa baba wa mataifa mengi. Na kama Mungu asingemwondoa Yusufu kutoka kwenye familia
ya Yakobo, basi Yusufu mwishowe angeuawa tu.
Madhara ya ndoa za wake wengi bado yanaiandama jamii ya binadamu hata leo. Katika jamii yetu, ndoa za wake wengi
au wanaume kupenda wanawake ambao sio wake zao husababisha umaskini kwa familia, umaskini ambao ungeweza
kuepukwa kama watu wangefuata misingi ya ndoa, kama ilivyoasisiwa na Bwana Mungu tangu zamani za uumbaji wa
mwanadamu. Sote ni mashahidi jinsi jamii yetu inavyopambana na tatizo sugu la ndoa za wake wengi na tatizo la
‘nyumba ndogo’ bila mafanikio. Uvunjifu huu wa maadili na misingi ya ndoa kamwe hautusaidii, ila ni mwanzo wa
uharibifu mkubwa wa kizazi cha binadamu.
Jifunze na kusoma kwa makini maoni ya wengine
|