Taasisi ya Ndoa na Sheria ya Ndoa Tanzania (13)
Ndoa katika mfumo wa Torati (sheria)

Juma lililopita tulimalizia kwa kuangalia mazingira yaliyomfanya Yakobo mtoto wa Isaka na mjukuu wa Baba
wa Imani, Mzee Ibrahimu, kuoa mke zaidi ya mmoja,  kinyume na ilivyokuwa   mwanzo,  tangu enzi za   
Adamu na Hawa. Leo tunaanza kuangalia maendeleo na  matatizo  katika Taasisi ya  Ndoa,  ndani ya mfumo
wa Torati.

Matatizo yaliyoikumba familia ya Yakobo, yakitawaliwa na chuki kati ya wake zake na watoto wao, yalimfanya mtoto wa
Yakobo na Raheli, Yusufu kuuzwa na ndugu zake kwa kikosi cha askari wa Misri  na hivyo wakaondokana kabisa na
Yusufu, ambaye ingawa alikuwa kipenzi cha baba, lakini alichukiwa sana na ndugu zake.

Ndugu zake, hata hivyo, walimdanganya baba yao kuwa mdogo wao Yusufu aliuawa na mnyama mkali na walitoa
kanzu yake kama ushahidi wa madai yao. Baba yao Yakobo pamoja na kumwombolezea sana mwanawe Yusufu, lakini
hatimaye  alisahau. Miaka mingi sana ikapita , akijua kuwa ni kweli mtoto wake alikuwa ameuawa na mnyama.

Kama tunavyosoma kwenye Biblia, Yusufu pamoja na vikwazo vyote alivyokutana navyo kama mtumwa nchini Misri,
baadaye Mungu alimfanikisha na kuwa mkombozi wa familia yake, pale njaa ilipoikumba familia ya Yakobo katika nchi
ya Kanaani.

Ukimya wa miaka 430

Kwa miaka  zaidi ya 400 nchini Misri, familia ya Yakobo iliongezeka kutoka watu 72 na kufikia watu zaidi ya milioni tatu,
wakati wanatolewa na Mungu kwa mkono wa Musa kurudi nchini Kanaani. Katika kipindi chote hicho ambacho familia
ya Yakobo iliishi nchini Misri, hapakuwa na mawasiliano kati yao na Mungu, kama ilivyokuwa desturi ya Mungu na watu
wake huko nyuma.

Kwa nini Mungu aliamua kuambatana na Yusufu?
Hapo nyuma tumeona kuwa sababu ya msingi ya Yusufu kuchukiwa na ndugu zake ni kule kuonekana kupendwa sana
na baba yake kuliko ndugu zake wengine. Pia Yusufu alikuwa na tabia ya kuwasimulia wazazi wake pamoja na kaka
zake maono na ndoto zake, ambazo zilionesha kwa dhahiri kuwa familia yao yote ingekuwa chini ya himaya yake siku
moja. Ingawa hatua hiyo sio tu kwamba iliwaudhi kaka zake wakubwa, lakini pia haikumpendeza hata baba yao. Siku
moja baba yao Yakobo alisema maneno haya:
“...Baba yake akamkemea akamwambia, ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja
tukusujudie hata nchi? Ndugu zake wakamhusudu, bali baba yake akalihifadhi neno hilo” (Mwanzo 37:10-11).

Swali la kujiuliza hapa ni  je, kwa nini Mungu aliamua kujifunua  kwa Yusufu kati ya watoto wengi wa Mzee Yakobo? Na
je! Kuna uhusiano wowote kati ya maisha ya Yusufu na mazingira ya ndoa ya baba yao?

Kwanza kabisa, yale yaliyokuwa yanajitokeza kwa Yusufu ulikuwa ni mchakato wa Mungu kutimiza ahadi yake
aliyomwapia Ibrahimu kuwa angeendelea kutimiza agano lake kupitia vizazi vyake. Pili, mazingira ya Yusufu kuota
ndoto ambazo ziliendelea kutengeneza chuki kati yake na ndugu zake yalikuwa yanalenga kukamilisha unabii ambao
Mungu alimwambia Ibrahimu kuhusu taifa litakalotokana naye kwenda kuishi nchini Misri kwa takriban miaka minne.
Unabii huo ulisema:
“Bwana akamwambia Abrahamu, ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi
isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa lile, watakaowatumikia,
nitawahukumu; baadaye watatoka na mali nyingi”, (Mwanzo 15:13-14).

Unabii huu ulikuwa lazima utimizwe. Kwa upande wa Taasisi ya Ndoa, je, kuna uhusiano wowote na mchakato wa
kumfanya Yusufu kubeba jukumu la kutimiza ule unabii? Jibu ni Ndio. Kuna sababu  ambayo kutokana na mazingira ya
ndoa ya Yakobo ya wake wawili, yaani Lea na mdogo wake Raheli, Yusufu ambaye ni mtoto wa Raheli ana uhalali wa
kuwa mtoto halali.

Kule nyuma tuliona kuwa agano la Mungu juu ya kumfanya Ibrahimu baba wa mataifa lingeingia kasoro pale ambapo
Ibrahimu alikubaliana na ushawishi wa mke wake wa kumtaka Mzee Ibrahimu azae na mjakazi wake Hajiri.Mungu
hakukubaliana na mpango huo wa kibinadamu na kwa hiyo alihakikisha Ibrahimu anapata mtoto halali kutoka kwa mke
wake wa halali Sara.

Hapa tunaona kuwa Mungu anaheshimu sana ndoa  na huhakikisha baraka zake zinafuata wahusika, iwapo
wataendelea kuwa wavumilivu. Kuhusu watoto wa Isaka, tuliona kuwa Mungu aliondoa haki ya uzaliwa wa kwanza
kutoka kwa Esau, kwenda kwa Yakobo. Hata hivyo, mpango huo ulikamilishwa kwa kuingiza hila za kibinadamu, lakini
lengo la Mungu lilitimia. Na hata kama ujanja wa kibinadamu usingetumika,  bado Mungu angehakikisha kuwa mpango
huo unatimia kwa njia zozote zile halali.

Lakini lazima tukumbuke kuwa Mungu ndiye anayejua maisha yajayo ya kila mtu hapa duniani. Na kwa upande wa
Esau, tunaona kuwa kule Mungu kumuondolea haki ya uzaliwa wa kwanza kulikuwa na mantiki.

Tumeona tangu mwanzo kuwa ushahidi wa mtu kukosa uhusiano mzuri na  Mungu ni kujiingiza katika ndoa za wake
wengi. Hali hii imeendelea hata kwa Esau kama tunavyosoma kwenye Biblia:
“Hivi ndivyo vizazi vya Esau, ndiye Edomu.
Esau alitwaa binti za Kanaani, kuwa wakeze”,(Mwanzo 36:1-2).  
Kule kwa Esau kujiingiza katika ndoa za wake wengi, hii
inatuonesha kuwa Mungu alijua kuwa Esau asingefuata mapenzi ya Mungu na hivyo mpango wake wa kuwa na taifa na
watu wanaomheshimu na kumwabudu ungeingia dosari.

Sasa tukirudi kwenye maisha ya Yakobo na familia yake na hasa mtoto wake Yusufu, tunaweza kusema yafuatayo:  
Wakati nachambua mazingira ya ndoa ya Yakobo, tuliona kuwa Yakobo tangu mwanzo hakudhamiria kamwe moyoni
mwake kuoa mke zaidi ya mmoja, isipokuwa alipatikana na hali hiyo kwa sababu ambazo yeye hakuwa  na uwezo wa
kuzizuia.

Kimsingi, ndoa inahitajika ridhaa ya wahusika, yaani mume na mke. Kwa Yakobo kama tulivyoona hapakuwa na ridhaa  
ya kumwoa Lea. Unaweza kuona kuwa Yakobo alikuwa na haki ya kumwoa Raheli, kwa sababu ndiye aliyekuwa
chaguo lake tangu mwanzo. Kwa kuangalia uhalali wa ndoa, Raheli ni mke halali wa Yakobo kwa sababu ndiye
aliyempenda kwanza. Na Mungu kama tulivyosema hapo juu ni kwamba ahadi za Mungu hufuata ndoa halali ambazo
kuwepo kwake kumefuata taratibu zote zinazofaa na kufuata misingi ya ki-Biblia.

Mungu alijua moyo wa Yusufu

Mungu kuamua kuendeleza agano lake na Yusufu, alizingatia usahihi wa Yusufu ambaye ni mtoto wa Yakobo kutoka
kwa Raheli. Kwa kufuata mapenzi ya Yakobo kwa Raheli na Yusufu akawa ndio mtoto wao wa kwanza, basi Mungu
alikuwa na sababu ya msingi kindoa kuelekeza uhusiano wake katika kutimiliza lile agano lake na Ibrahimu kwa njia ya
kumbariki Yusufu.  Pili ni kwamba, Mungu ajuaye mioyo ya watu, alijua kuwa Yusufu ndiye ambaye angeweza kuwa
msaada mkubwa katika mwendelezo mwema wa taifa la Israeli, ambalo Mungu alikusudia kuliunda kutokana na agano
lake na Ibrahimu.

Maisha ya Waisraeli nchini Misri

Mungu alimtanguliza Yusufu nchini Misri ili awe hifadhi ya familia ya baba yake baadaye na hivyo kutimiza maandiko
tuliyoyasoma, kuwa Wayahudi wangeishi kule miaka 400 kama watumwa.

Sababu pekee ambayo Mungu aliisema kuhusu familia ya Yakobo na hatimaye taifa lote kuwa chini ya utumwa, ni
kuwa kukaa kwao huko nchini Misri  kwa miaka 400, kungewafanya wao kuwa  matajiri kwa sababu siku ya kutoka
wangetoka na mali nyingi.

Lakini hayo yote yamewezekana kwa sababu Mungu aliheshimu misingi ya ndoa kwa kuamua kuibariki ndoa ya
Yakobo na Raheli, kama alivyofanya kwa Ibrahimu, Isaka. Kwa kifupi watu wote hawa wake zao walikuwa tasa, lakini
kwa sababu ndoa zilikuwa ni ndoa zilizozingatia msingi wa mke mmoja kwa mume mmoja, Mungu alihakikisha
anazibariki,  ili kuonesha kuwa kwake hakuna lisilowezekana. Familia ya Yakobo ambapo aliingia nchini Misri ikiwa na
watu 72, iliendeleza kizazi cha Ibrahimu kwa muda wa miaka mia nne  na kuwa taifa kubwa ambalo, baadaye liligeuka
kuwa tishio kwa taifa la Misri.

Tangu familia ya Yakobo ilipoingia Misri Katika miaka yote hiyo, hatuna habari za kuongezeka kwao na wala hakuna
habari zilizoandikwa kuhusu kuendelezwa kwa misingi ya ndoa, tunachojua ni kwamba watu hao 72, waliendelea
kuoana wao kwa wao na kuzaana  mpaka idadi yao ilipofikia watu zaidi ya milioni mbili, wakati wanaondoka nchini Misri.

Kuanza kwa Torati

Falsafa ya sheria (Jurisprudence) inasema kuwa sheria ipo ili kuhakikisha kizazi cha binadamu kinaendelea kuwepo.
Binadamu mwenye akili anaweza kufikiria hali ya maisha ya binadamu duniani ingekuwaje  bila kuwa  na mfumo wa
sheria. Ni dhahiri, kizazi cha binadamu kisingekuwepo; kwa sababu bila sheria, wanadamu wangeendelea kuuana na
mwisho wake, wote wangetoweka.

Baada ya Mungu kuwatoa wana  wa Yakobo (Israeli) kutoka Misri, tayari walikuwa ni jamii kubwa ambayo kuisimamia
bila sheria ingekuwa vigumu sana. Mungu kupitia Musa aliweka mfumo wa sheria akianzia na zile amri kumi, ambazo
ziliendelea kutungiwa sheria ndogo ndogo hadi kufikia zaidi ya sheria 600. Sheria na kanuni zote hizo zilikuwa na lengo
moja tu, nalo ni kumsaidia binadamu kuwa na uhusiano mzuri na Mungu    pia  na binadamu mwenzake.

Katika  hizo amri kumi na sheria zingine zote, misingi ya ndoa iliendelezwa. Tukiangalia amri 10, ni kwamba amri nne  
za kwanza  zinamtaka mwanadamu afanye mambo ambayo Mungu anataka au asifanye mambo ambayo Mungu hataki.
Kwa maneno mengine, sheria hizo nne za kwanza zililenga kudumisha uhusiano mwema kati ya Mungu na wanadamu,
kwa faida ya wanadamu wenyewe.

Amri sita zilizobaki zililenga kudhibiti mahusiano kati ya mtu na mwenzake au mtu mmoja na jamii na hivyo kumfanya
kila mtu aishi kwa amani na raha mustarehe kabisa bila bugudha yoyote. Kama kawaida sheria bila adhabu sio sheria.
Hatimaye Mungu, kupitia Musa aliendelea kutengeneza kanuni za utekelezaji wa amri hizo kuu 10 na pia kuweka
adhabu kama njia ya kuwaadhibisha wakosaji ili wajirekebishe na wasirudie tena.

Kati ya amri hizo 10, zipo zile ambazo lengo lake kuu lilikuwa ni kuendeleza misingi ya ndoa kama ilivyokuwa wakati wa
Ibrahimu, Isaka na Yakobo, ambao walibakia kuheshimiwa na taifa lote la Israeli, kama baba na babu zao wa imani na
waanzilishi wa taifa la Israeli mpaka leo. Kati ya hizo amri 10, amri tatu zilihusu mahusiano ya kifamilia moja kwa moja.
Amri ya tano, ilikusudiwa kudumisha heshima kati ya wazazi na watoto wao.

Hapa mtu yeyote mwenye umri wa utu uzima alitakiwa kuwaheshimu wazazi wake, kama bado walikuwa hai. Amri ya
saba (maarufu kama amri ya sita), ililenga kuzuia zinaa kati ya wanadamu wenye ndoa. Ilisema Usizini! Amri ya 10,
pamoja na mambo mengi, ilikataza mtu- hasa mwanaume asitamani mke wa mwenzake.  Siku zote lengo la sheria huwa
ni jema, lakini sheria ni kikwazo kwa binadamu kwa sababu huiona kama ni mkakati wa kumnyima uhuru wa kufanya
vile anavyotaka.
Jisomee makala ili uelimike na kupanua
ufahamu