| Je, ni kweli Serikali ya awamu ya nne ina udini? Na Sakofu Sylvester Gamanywa Zimekuwepo hisia miongoni mwa baadhi ya madhehebu ya Kikristo kwamba Serikali ya awamu ya nne imeanza kuonesha udini katika utendaji wake. Kigezo kikuu kinachotumiwa katika madai haya ni kuteuliwa kwa waislamu wengi kushika madaraka ya uongozi wa juu. Hofu iliyotawala miongoni mwa waliotawaliwa na dhana hii ni tafsri kwamba huu ni mkakati maalum wa kuweka waislamu wengi madarakani ambao hatimaye wataifanya Tanzania iwe nchi ya Kiislamu. Je! Hivi ni kweli Serikali ya sasa imejaa udini? Vigezo vinavyotumika kueneza uvumi huu vina mantiki? Je! Hivi ni haki na halali kuanza kumshutumu Rais ati kwa sababu kuna idadi kubwa ya Waislamu katika Serikali yake? Hoja hii imedhamiria kujibu maswali haya na mengineyo muhimu kwa nia ya kujipanga upya kimtazamo: Si jambo rahisi kuifanya Tanzania nchi ya Kiislamu Nimeamua leo kuleta hoja hii nyeti kwa sababu nimekuwa nikisumbuliwa na baadhi ya wakristo wenzangu, hususan viongozi wa madhehebu ya Kikristo, wakitaka kuniaminisha kwamba Serikali ya awamu ya nne ina udini. Aidha, baadhi yao wamenikumbusha mambo ya zamani ya mikakati ya OIC na IAO ilivyowahi kuitikisa nchi yetu kisiasa. Kwa kuwa mimi mwenyewe nimekuwa mwanaharakati wa siku nyingi wa kutetea juhudi za kudumisha amani na utulivu, pamoja na uhuru wa kuabudu kwa kila dini katika jamii; nimeanza kushinikizwa kuendeleza uanaharakati wangu kuhusu madai waliyo nayo dhidi ya uteuzi wa watendaji wa Serikali ya awamu ya nne. Kwa hiyo basi, kupitia makala haya, napenda kwanza kuwaondolea wasiwasi na hofu wakristo wenzangu msikubali kujiruhusu kutawaliwa na hisia za jinsi hii katika jamii. Nasema hivi kwa sababu, hata kama huko zamani ziliwahi kuwepo dalili za udini katika baadhi ya watendaji wa Serikali zilizopita, tusisahau kwamba hivi sasa mambo mengi yamebadilika sana, tena ghafla. Hizi ni enzi mpya za utandawazi ambamo kila kitu si siri tena. Kwa kadri mwingiliano wa kijamii kutoka nje unavyozidi kuongezeka, ndivyo hata fikra za kujaribu kuifanya Tanzania iwe nchi ya kidini pia zinazidi kufifia kama sio kufa kabisa. Baada ya maelezo yangu hapa juu, ningependa kutahadharisha mapema kwamba, madai kwamba kuteuliwa waislamu wengi kushika madaraka ni dalili za kutaka kuifanya Tanzania iwe nchi ya Kiislamu, si sahihi. Mtazamo wa jinsi hii si mzuri, hususan kwa wakristo wenzangu. Sote ni mashahidi wa kweli kwamba nchi hii imekuwa ikiongozwa kwa misingi ya Katiba. Kila Mtanzania anafahamu bayana kwamba, Serikali ya Nchi ni ya kisekula (Secular State); kwa maana kwamba Serikali haina dini wala haipo kupendelea dini moja dhidi ya nyingine. Kwa hivyo basi, nazidi kusisitiza kwamba si tafsiri sahihi kudai kwamba Rais ameteua watendaji wakuu serikalini kwa misingi ya udini. Ninaamini kwamba uteuzi wa Rais wetu umezingatia zaidi uwezo wa mtu na si dini anakotoka. Rais wetu si mgeni na hisia hizi za udini. Anafahamu kabisa kwamba hisia kali za udini kama zikiendekezwa hatimaye zinaweza kutupeleka mahali pabaya. Wala hawezi kuthubutu kufanya makosa kama haya hapa mwanzoni mwanzoni tu wa utawala wake. Ni mapema sana kuhukumu mambo Hapa napenda kukumbusha kwamba Wakristo tunajulikana kwa utamaduni wa kutumia hoja katika kusema, badala ya kutawaliwa tu na hisia za jazba na tafsiri zisizothibitishwa. Kwa busara zile zile, lazima tukubali kwamba hivi sasa ni mapema mno kuwahukumu walioteuliwa kabla hata hawajaanza kufanya kazi zenyewe walizoteuliwa kufanya. Lazima tuwape uhuru na nafasi walioteuliwa kuongoza nchi waoneshe uwezo wao. Nimeambiwa kwamba mkakati wa Waislamu kuwa wengi katika utawala ni wa kutaka kubadili Katiba ya Nchi na kuweka vipengele vya upendeleo wa kidini kwa dini moja dhidi ya dini nyingine. Na kwa sababu wao tayari watakuwa ni wengi wakati wa kupiga kura; basi agenda yao itapita bila kupingwa, kwa kisingizio cha Demokrasia. Hizi ni hisia kali sana za kidini na zisipodhibitiwa zinatishia amani na utulivu wa taifa letu. Bado napinga kwa kusema hisia hizi si sahihi kwa sababu bado hakuna ajenda ya kubadili Katiba iliyowasilishwa bungeni yenye mwelekeo wa kuifanya Serikali ivunje utamaduni wake wa kuwa ya kisekula kama ilivyo hivi sasa. Na kama ipo inakuja, basi tuisubiri ijitokeze. Narejea kusema tena kwamba si busara za Kikristo kuanza kueneza uvumi mitaani kwamba sasa tumeanza kutawaliwa kidini, kwa kuwa viongozi wa ngazi za juu wengi wao ni Waislamu. Tusubiri tuuone udini huo kama upo kweli, ukijitokeza kwa vitendo. Ni muhimu kuwa na ushahidi kamili ndipo tuseme. Tusikubali kueleweka vibaya kuwa sisi ndio wenye udini Napenda pia kuchukua fursa hii kutahadharisha juu ya dhana kwamba waislamu wengi wakiteuliwa kushika madaraka badala ya wakristo ni udini kwa upande mmoja; kisha tukasahau kwamba mtazamo huu unaweza kutafsiriwa vibaya dhidi yetu kwamba nasi tumeanza kuonesha udini! Kama tutaendelea kuwatazama watendaji wanaoteuliwa na Rais kwa ‘jicho la dini’ wanakotoka; tayari nasi tutakuwa tumeangukia upande wa udini dhidi ya Waislamu! Lazima tukubali mabadiliko. Kama tutaendelea kufikiri kwamba wakristo wengi kutawala ndiko kutaifanya Tanzania isiwe nchi ya kidini; nadhani tutakuwa tumekosea kimtazamo. Maana wasio Wakristo nao wataendelea kutafsiri kwamba Tanzania ni nchi ya Kikristo, ati kwa sababu akina Mathayo na Yohana ndio waliojaa madarakani kuliko Issa na Yahaya. Tukumbuke kwamba huko nyuma yaliwahi kuwepo madai kutoka baadhi ya vikundi vya Kiislamu vikishinikiza tafsiri kwamba Tanzania ni ‘nchi ya Kikristo’, ati kwa sababu wakristo wengi ndio waliojaa madarakani kuliko Waislamu. Sisi nasi tukawa tunajitetea kwa hoja kwamba wakristo wengi huwepo madarakani kutokana na uwezo wao na si kwa sababu ni wakristo. Tukatafsiri kwamba wenye madai ya jinsi hii wana udini. Haya sasa, idadi ya Waislamu inapoongezeka katika utawala kuliko ilivyokuwa huko zamani, baadhi yetu tumeangukia katika mtego ule ule wa kutafsiri kuwa huu ni udini. Tusipojirekebisha tayari tutawapa nguvu wasio wakristo ‘kutubatiza’ jina la ‘udini,’ hali ambayo hata kama tulikuwa na hoja za msingi tutapuuzwa. Tutaitwa ‘Mujahidina wa Kikristo’! Sidhani kama huko ndiko tunakotaka kwenda. Itaendelea toleo lijalo. |