KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA

TAMKO  LA  BARAZA LA MAASKOFU WA KKKT KUHUSU
UANZISHWAJI WA MAHAKAMA YA KADHI TANZANIA BARA.

1.0        Sisi Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) pamoja na Halmashauri
Kuu ya Kanisa, tuliokutana Chuo Kikuu Kishiriki cha Makumira, Arusha, tangu tarehe 9 Agosti
2006, pamoja na mambo mengine, tumetafakari kwa roho ya utume wetu kwa taifa hili, juu ya
uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, Tanzania Bara.

2.0        Tunatambua kwa dhati na fahari kubwa, kuwa Serikali yetu haina dini na kwamba huu
umekuwa msingi imara wakuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Aidha, tunatambua kuwa
Serikali yetu na mihimili yake yote muhimu inao wajibu wa kuhakikisha kuna kutenganisha
mambo ya dini na mambo ya Serikali ili kulinda mshikamano wa kitaifa.

3.0        Siku za karibuni, Vyombo mbalimbali vya Habari na watu binafsi wenye dhamana katika
jamii, vimekuwa vikijitahidi juu ya uwezekano wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi. Suala hili
linapojadiliwa  linakuwa na mwelekeo unaoonesha kuwa kuna mvutano wenye hisia kali
zinazoweza kuleta na kubomoa amani ya jamii kwa sababu linagusa hisia za kidini na itikadi.

4.0        Tunatambua kuwa, vyama vya siasa katika kujinadi kwa wanachama na wapiga kura wake,
vinazo katika ilani zake, ahadi zinazolenga kuanzisha mchakato wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi
hapa Tanzania Bara.

5.0        Mafafanuzi ambayo yametolewa kuhusu kazi na wajibu wa Mahakama ya Kadhi
yameonesha kuwa Mahakama hii itashughulikia:

i)        Kufunga ndoa za Kiislam na kuzihakiki uhalali wake
ii)        Masuala ya talaka
iii)        Mirathi
iv)        Dini (tawheed)
v)        Ibada na hadhi ya waislam

Mambo haya ni ya msingi katika ustawi wa familia na jamii kwa ujumla.

6.0        Hata kwa mafafanuzi haya, tunatambua kuwa jamii ya Watanzania inazo ndoa mseto,
familia mseto ni mali zinazomilikiwa kwa misingi ya imani mseto. Mseto huu ni msingi wa
mshikamano  katika jamii na uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi utabomoa kwa hakika nguzo hii
muhimu ya maridhiano pale matatizo yatakapotokea katika familia husika.

7.0        Msukumo wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi unaibua mashaka na maswali matatu ya
msingi:

1.        Tangu tupate uhuru, Serikali imesisitiza kutokuwa na dini na faida zake tumeziona. Ni kwa
faida gani leo, tunalishawishi Bunge letu kutunga sheria ya kuunda Mahakama ya Kadhi?

2.        Vyombo vilivyoundwa kwa mujibu wa sheria, huendeshwa kwa kodi ya Watanzania wa dini
zote. Ni kwa nini leo hii tunadiriki kujaribu kujadili kuruhusu kisheria, kundi moja la kidini,
kuendesha ofisi yake na Mahakama yake, kwa kutumia fedha za walipa kodi wote?

3.        Je, kuwaundia waislamu Mahakama yao hakutaweka mwanya unaoweza kuwafanya kudai
nafasi ya pekee katika utawala wa nchi hii? Na je, Mahakama hii itatuhakikishiaje kuwa haki za
wanawake zitahifadhiwa?

HITIMISHO:
Kwa kuzingatia mawazo haya, Sisi  Maaskofu wa KKKT na Halmashauri Kuu ya Kanisa zima,
tunawiwa na dhamiri zetu kuangalia kuwa, uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi ni jambo la hatari
kwa amani, umoja na mshikamano wa taifa letu. Aidha, uanzishwaji wa mahakama hii
kutaidhoofisha Katiba ya Nchi  inayobainisha wazi kutenganisha mambo ya dini na Serikali, kwa
sababu Serikali yetu haina dini. Hivyo basi, tunasihi Bunge letu lisikubali kamwe kuruhusu
uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi. Tanzania yenye amani ni tunda la dini, itikadi, makabila, rangi
na jinsia zote.

MUNGU IBARIKI TANZANIA

Ni sisi Maaskofu wa KKKT.

limesainiwa na

Askofu Dk. Samson Mushemba,
MKUU, KKKT
K.n.y  Maaskofu wote wa KKKT.
The Word And Peace Organization, Loliondo Street Plot 29, Kurasini
P.O. Box 6178, DAR ES SALAAM

Phone: 255 22 2850234 Fax: 255 22 2851266
Email:
info@wapotz.org